Lukaku ajibu baada ya bosi wa Inter Milan kukeji uzito mkubwa wa mwili wake

Lukaku alisema, "Niangalie vizuri zaidi , niko katika hali nzuri, mama mia!"

Muhtasari

•Marotta alisema kuwa uzito mkubwa wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 amefanya mchezo wake kuwa chini katika siku za hivi majuzi.

•Pia alidokeza kuwa jereha ndogo ambalo Lukaku alipata kwenye mashindano ya Kombe la Dunia  liliathiri mchezo wake.

Romelu Lukaku
Image: HISANI

Mkurugenzi Mtendaji wa klabu ya Inter Milan, Beppe Marotta ametoa maoni makali kuhusu mwili wa mshambulizi Romelu Lukaku.

Akizungumza na Sky Sport Italia siku ya Jumatano, Marotta alisema kuwa uzito mkubwa wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 amefanya mchezo wake kuwa chini katika siku za hivi majuzi.

“Lazima niseme ana kilo 103 za kubeba, hivyo anatakiwa kuwa na umbo kamilifu ili aweze kucheza vizuri na bado hajafika hapo," alisema.

Siku za hivi majuzi, Lukaku hajakuwa akishirikishwa katika dakika nyingi za mechi za Inter. Mshambuliaji huyo amecheza mechi moja tu kamili na kufunga mabao manne kwenye mashindano yote.

Marotta hata hivyo ameeleza matumaini yake kuwa mshambulizi huyo amejikita katika kufikia hali ambayo anahitajika kuwa katika ili kuhusishwa katika dakika nyingi za michuano ya klabu hiyo ya Italia.

"Anafika hapo na kocha ndiye mtu bora wa kutathmini jinsi anafanya na jinsi anavyopaswa kutumika. Siku hizi mechi hudumu takriban dakika 100, kwa hivyo wachezaji wanaotoka kwenye benchi wanaweza kuwa muhimu kama wachezaji wenzao.

Mkurugenzi huyo pia alidokeza kuwa jereha ndogo ambalo mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ubelgiji alipata kwenye mashindano ya Kombe la Dunia mwishoni mwa mwaka jana liliathiri mchezo wake.

"Kwa bahati mbaya, shida nyingine ya msimu huu mbaya ni Kombe la Dunia, ambalo lilikuwa katikati ya kipindi cha kwanza cha msimu.

Ninaona kwamba ushiriki wa Kombe la Dunia uliathiri wachezaji wengi, wengine wanahisi zaidi kuliko wengine, na Lukaku alikuwa na jeraha ambalo lilimaanisha kwamba alipunguzwa na kuwa sanamu tu kwenye mashindano hayo,” alisema.

Lukaku, ambaye awali amewahi kuchezea vilabu vikubwa vya EPL kama Chelsea, West Brom, Everton na Manchester United, aliingia katika dakika ya 58 kwa Edin Dzeko na kufunga bao la ushindi la Inter-Milan dhidi ya FC Porto kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa iliyochezwa siku ya Jumatano usiku.

Huku akijibu maoni ya mkurugenzi wa Iklabu yak baada ya mechi, alisema kwa mzaha, "Wow, niangalie vizuri zaidi .. niko katika hali nzuri, mama mia!"