Messi asimamishwa kazi PSG kwa safari isiyoidhinishwa ya kwenda Saudi Arabia

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwaka jana amepigwa marufuku kucheza au kufanya mazoezi na timu.

Muhtasari

•Mwanasoka huyo aliruka mazoezi ya PSG ili kuenda Saudi Arabia kama sehemu ya jukumu lake kama balozi.

•Kufuatia hayo, klabu hiyo ya Ufaransa imeripotiwa kumsimamisha kazi Lionel Messi kwa wiki mbili bila malipo.

Image: HISANI

Staa wa soka Lionel Messi ameadhibiwa na klabu yake ya sasa ya Paris Saint-Germain kufuatia safari yake ya kwenda Saudi Arabia bila kibali.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 35 alionekana jijini Riyadh, Saudi Arabia siku ya Jumatatu na aliripotiwa kuruka kipindi cha mazoezi ya PSG ili kufanya ziara hiyo kama sehemu ya jukumu lake kama balozi wa utalii katika hatua ambayo haikuidhinishwa na kocha wake Christopher Galtier.

Kufuatia hayo, klabu hiyo ya Ufaransa imeripotiwa kumsimamisha kazi Lionel Messi kwa wiki mbili bila malipo.  Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwaka jana amepigwa marufuku kucheza au kufanya mazoezi na timu.

Atakosa mechi zijazo za Ligue 1 dhidi ya Troyes na Ajaccio, lakini anaweza kurudi kwa mechi dhidi ya Auxerre mnamo Mei 21. PSG wapo kileleni mwa jedwali la Ligue 1  wakiwa na pointi 75 kutokana na mechi 33 walizocheza. Messi alianza katika mechi ya hivi majuzi dhidi ya Lorient ambapo PSG iliyochapwa 3-1 nyumbani.

Raia huyo wa Argentina yuko katika miezi ya mwisho ya mkataba wake wa miaka miwili na viongozi hao wa Ligue 1. Hapo awali alipewa mkataba wa mwaka mmoja wenye thamani ya £400m kuichezea Al Hilal ya Saudi Arabia, ingawa hakuna dalili kama ofa yao ilikuwa na uhusiano wowote na safari yake. Messi tayari anahudumu kama balozi wa utalii katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Utalii wa Saudi Arabia Ahmed Al-Khateeb alitoa taarifa kwenye Twitter akimkaribisha Messi na pia kuchapisha picha za mshindi huyo wa Kombe la Dunia la mwaka jana, saa chache tu baada ya kucheza dakika 90 za kichapo cha PSG cha 3-1 dhidi ya Lorient nyumbani.

"Nina furaha kumkaribisha Messi na familia yake nchini Saudi ili kufurahia maeneo ya kitalii ya ajabu na uzoefu halisi," Al-Khateeb aliandika.

Aliongeza, "Tunakaribisha wageni kutoka kote ulimwenguni kupata safari ya kipekee ya Saudi Arabia na ukarimu wake."