Ndovu astarehe juu ya mti tena, kusalia kileleni kwa angalau wiki tatu

Ushindi wa Jumamosi usiku uliwapeleka wanabunduki kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 64.

Muhtasari

•City na Liverpool ziligawana pointi kwani hakuna hata mmoja aliyeweza kumshinda mpinzani wake, mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

•Timu tatu zinazoongoza zitacheza tena mwisho wa Machi  kwani ligi ikikaribia kuchukua mapumziko ya kimataifa.

Image: INSTAGRAM// ARSENAL

Mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Uingereza zilipata kuchezwa katika viwanja tofauti wikendi ambapo klabu ya Arsenal FC ilipata kupanda tena juu ya jedwali msimu huu.

Vijana wa Mikel Arteta walicheza mchezo mgumu dhidi ya Brentford uwanjani Emirates siku ya Jumamosi jioni ambapo walirudi nyumbani na pointi tatu kufuatia bao nzuri la Kai Havertz bao katika dakika za lala salama na kufanya matokeo kuwa 2-1.

Wanabunduki walikuwa wa kwanza kufunga bao kupitia kwa k iungo Declan Rice katika dakika ya 19 ya mechi hiyo ya kusisimua kabla ya mshambuliaji  wa Kongo Yoane Wissa kuwasawazishia The Bees katika dakika za mwisho za kipindi cha kwanza.

Mechi hiyo iliyowafanya mashabiki wa Arsenal kushikilia roho zao nusura imalizike kwa sare ya 1-1 kabla ya mchezaji wa zamani wa Chelsea, Kai Havertz, ambaye yuko katika fomu nzuri sana, hatimaye kufunga bao zuri la kichwa dakika ya 86.

Ushindi huo wa Jumamosi usiku uliwapeleka wanabunduki  kileleni mwa jedwali wakiwa na pointi 64 wakisubiri matokeo ya mechi ya Manchester City na Liverpool Jumapili ili kujua kama watasalia kileleni.

Kweli, siku ya Jumapili ilifika na wababe hao wawili wa Ligi Kuu ambao wamekuwa wakitawala nchini Uingereza kwa miaka kadhaa iliyopita walikabiliana katika mechi ya kusisimua sana iliyochezwa kwenye uwanja wa Anfield mwendo wa saa moja kasorobo jioni.  

Baada ya dakika 90 kumalizika na kuongezwa muda, timu zote ziligawana pointi kwani hakuna hata mmoja aliyeweza kumshinda mpinzani wake, mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1.

Beki John Stones alianza kuifungia Manchester City dakika ya 23 kabla ya kiungo wa Argentina Alexis Mac Allister kuisawazishia Liverpool katika dakika ya 50.

Sare hiyo iliirudisha Liverpool kwenye nafasi ya pili, ikilingana pointi 64 na Arsenal lakini nyuma kwa mabao. Kwa upande mwingine, Man City ilianguka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 63.

Timu hizo tatu zinazoongoza zitacheza tena mwisho wa Machi  kwani ligi ikikaribia kuchukua mapumziko ya kimataifa.

Man City watawakaribisha Arsenal katika uwanja wa Etihad mnamo Machi 31 huku Liverpool wakimenyana na Brighton tarehe hiyo hiyo.