UCL DRAW: Jinsi vilabu vimepangwa kwa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa

Mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa mnamo Februari 13 na Februari 14, 2024.

Muhtasari

•Droo ya Ligi ya Mabingwa ya hatua ya 16 bora ilifanyika siku ya Jumatatu alasiri, Disemba 18 kwenye Jumba la Soka la Uropa jijini Nyon, Uswizi.

•Vinara wa sasa wa Ligi Kuu ya Uingereza Arsenal watakapomenyana na FC Porto ya Ureno.

Image: HISANI// UCL

Vilabu mbalimbali vya Uropa vilivyomaliza katika nafasi mbili za kwanza katika vikundi vyao tofauti vya Ligi ya Mabingwa 2023/24 sasa vinajua watakutana na nani katika hatua ya 16 bora.

Droo ya Ligi ya Mabingwa ya hatua ya 16 bora ilifanyika siku ya Jumatatu alasiri, Disemba 18 kwenye Jumba la Soka la Uropa jijini Nyon, Uswizi. Haya yanajiri siku chache tu baada ya awamu ya makundi kukamilika wiki iliyopita huku klabu 16 zikipiga hatua inayofuata.

Kufuatia droo hiyo, mechi ya mkondo wa kwanza kati ya nane zitachezwa Februari 13, 2024 na Februari 14, 2024 wakati vinara wa sasa wa Ligi Kuu ya Uingereza Arsenal watakapomenyana na FC Porto ya Ureno.

FC Copenhagen ya Denmark waliomaliza katika nafasi ya pili katika kundi la kwanza watamenyana na washindi wa EPL 2022/23 Manchester City tarehe sawa huku wababe wa soka wa Italia, Napoli wakiwakaribisha Barcelona.

PSG ya Ufaransa itaikaribisha Real Sociedad ya Uhispania huku Inter Milan ya Italia ikiwakaribisha Atletico Madrid ya Uhispania.

Miamba ya soka ya Uholanzi PSV Eindhoven itaikaribisha Borrussia Dortmund ya Ujerumani huku Lazio ya Italia ikiikaribisha Bayern Munich.

Klabu nyingine ya Ujerumani, RB Leipzig itamenyana na Real Madrid ya Uhispania ambayo inashikilia mataji mengi zaidi katika mashindano ya Ulaya.

Mechi ya mkondo wa pili itachezwa Machi 5-6 au Machi 12-13.