HATUA MWAFAKA

Okutoyi kujiunga na chuo kikuu cha Auburn Marekani

Okutoyi, 18, ni mhitimu wa shule za msingi za Loreto Convent na Mbagathi jijini Nairobi.

Muhtasari

•Anatazamiwa kujiunga na Auburn mnamo Januari 2023.

•Okutoyi alifungua ukurasa mpya katika historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kutawazwa bingwa katika hafla ya Grand Slam.

Angella Okutoyi
Angella Okutoyi
Image: HISANI

Mchezaji mahiri wa tenisi nchini Kenya, Angella Okutoyi, hatimaye amechagua chuo atakachojiunga nacho katika azma yake ya kuwa bingwa wa dunia.

Katika chapisho kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Okutoyi alifichua kuwa atajiunga na Chuo Kikuu cha Auburn nchini Marekani.

"Nina furaha sana kutangaza kwamba nitaendelea na kazi yangu ya tenisi na masomo katika Chuo Kikuu cha Auburn! Shukrani kwa familia yangu, makocha, marafiki na kila mtu ambaye alinisaidia kufika hapa!" Okutoyi aliandika.

Okutoyi, 18, ni mhitimu wa shule za msingi za Loreto Convent na Mbagathi jijini Nairobi. Pia alihudhuria kituo cha Shirikisho la Tenisi la Kimataifa (ITF) nchini Burundi.

Anatazamiwa kujiunga na Auburn mnamo Januari 2023 baada ya kushiriki mashindano ya W15 Monastir nchini Tunisia mnamo Oktoba 17-23 na W15 Nairobi katika Klabu ya Karen Country jijini Nairobi mnamo Novemba 14-20.

Mnamo Septemba 6, alibanduliwa nje ya mashindano ya wasichana ya US Open baada ya kupoteza kwa Taylah Preston wa Australia.

Okutoyi alikuwa na matumaini ya kufika robofainali, hatua moja kutoka kwa juhudi zake za awali nchini Australia, ambapo alijitoa katika raundi ya tatu.

Okutoyi aliungana na mchezaji wa Uholanzi Rose Marie Nijkamp kushinda taji la Wimbledon Doubles mnamo Juni 20.

Wachezaji hao wawili waliokutana kwenye Instagram, waliwashinda Wakanada Kayla Cross na Victoria Mboko katika fainali ya michuano ya Wimbledon Open doubles Junior Championships katika All England Lawn.

Kisha mnamo Septemba 3, Okutoyi alishirikiana na Malwina Rowinska wa Poland kushinda J1 Repentigny Doubles katika Hifadhi ya Larochelle nchini Kanada.

Okutoyi alifungua ukurasa mpya katika historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kutawazwa bingwa katika hafla ya Grand Slam.