Wanyama afurahia wakati mzuri na mwanawe katika uwanja wa CF Montreal, Canada (+video)

"Nyakati kama hizi #Nimebarikiwa," mkewe alisema.

Muhtasari

•Wanyama ambaye anacheza katika nafasi ya kati alihusika katika mechi ya Jumapili huku klabu hiyo ya Kanada ikiwazima wapinzani wao.

•Mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham alionekana akiingia uwanjani na mwanawe huku Serah akiwarekodi. 

Mchezaji Victor Wanyama, mkewe Serah Teshna na mtoto wao
Image: INSTAGRAM// SERAH TESHNA

Familia ndogo ya nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Harambee Star, Victor Mugubi Wanyama ilitazama huku klabu yake ya CF Montreal Impact ikipata ushindi wa 3-2 dhidi ya Philadelphia Union siku ya Jumapili.

Wanyama ambaye anacheza katika nafasi ya kati alihusika katika mechi ya Jumapili huku klabu hiyo ya Kanada ikiwazima wapinzani wao. Mabao mawili ya mshambulizi Romell Quioto na Chinonso Offor yalifanikisha ushindi huo.

Mkewe Wanyama, muigizaji Serah  NdanuTeshna na mtoto wao mdogo walitazama mechi hiyo moja kwa moja kwenye uwanja wa Saputo.

Baada ya mechi, mchezaji huyo wa zamani wa Tottenham alionekana akiingia uwanjani na mwanawe huku Serah akiwarekodi. Wanyama bado alikuwa amevalia sare ya CF Montreal huku akitembea uwanjani na mwanawe.

"Nyakati kama hizi #Nimebarikiwa," Serah aliandika kwenye Instagram

Mwaka jana, Teshna aliweka wazi kwamba hayupo kwenye mahusiano ya umbali mrefu na mchumba wake Victor Wanyama.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Serah alifichua  amekuwa akiishi pamoja na mchezaji huyo wa Harambee Stars.

Mbabe huyo wa uigizaji alikuwa amerejea nchini kwa siku chache mnamo mwezi Mei kwa minajili ya kikazi.

"Sipo kwenye mahusiano ya umbali mrefu. Kusema kweli tumekuwa pamoja kila wakati, tunaishi pamoja. Niko hapa kwa sababu ya kazi ninayofanya hapa kisha nirudi," Serah alisema.

Serah alisema kuwa alikusudia kuungana tena na familia yake punde baada ya kukamilisha kazi iliyomleta hapa nchini.

"Huwa hatuweki mambo yetu wazi lakini daima tuko pamoja katika kila jambo. Niko hapa kwa mradi huu tu lakini baada ya kumaliza ni lazima niungane tena na familia yangu," Serah alisema.

Kwa sasa Wanyama anaishi Canada ambapo anachezea klabu ya CF Montreal inayoshiriki katika Major League Soccer (MLS).

Wawili hao walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja Septemba mwaka wa 2021. Serah alitangaza habari za kuzaliwa kwa mtoto wao wa kiume siku 40 baada ya kujifungua.

“2021. Mungu alijitokeza na Kujionyesha. Tunayo furaha kushiriki safari hii ya ajabu na wewe. Mungu ndiye mkuu. #siku40ZaBabyCuddles," Teshna alitangaza mwezi Oktoba kupitia Instagram.

Muigizaji huyo alifichua kuwa amekuwa akipumzika kuigiza tangu alipojifungua. Alisema ana uhusiano wa karibu sana na mwanawe.