Gidi akosoa Sauti Sol baada yao kutishia kushtaki Azimio kwa kutumia wimbo wao bila idhini

Muhtasari

•Sauti Sol walilalamikia kitendo cha Azimio kutumia wimbo wao 'Extravangaza' katika tangazo la mgombea mwenza wa Raila.

•Mtangazaji huyo ambaye aliwahi pia kuwa mwanamuziki amependekeza kuwa badala yake bendi hiyo ingetumia fursa hiyo kujinufaisha kifedha.

Mtangazaji Joseph Oyoo almaarufu Gidi na Bendi ya Sauti Sol
Mtangazaji Joseph Oyoo almaarufu Gidi na Bendi ya Sauti Sol
Image: HISANI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi Gidi Ogidi amekosoa hatua ambayo bendi ya Sauti Sol ilichukua baada ya wimbo wao kutumika katika mkutano wa kisiasa wa Muungano wa Azimio la Umoja.

Siku ya Jumatatu Sauti Sol walilalamikia kitendo cha Azimio kutumia wimbo wao 'Extravangaza' katika tangazo la mgombea mwenza wa Raila, Martha Karua.

Bendi hiyo ilidai kuwa muungano huo haukuomba idhini ya kutumia wimbo wao na kutokana na hayo wakatishia kuchukua hatua za kisheria.

"Tungependa kufahamisha mashabiki wetu na washirika wetu kuwa hatuna uhusiano na kampeni za Azimio La Umoja ama vuguvugu /chama chochote cha kisiasa na wagombea urais wao, wagombea wenza wao na wagombea viti vingine. Hatujihusishi na siasa," Bendi hiyo ilitangaza kupitia taarifa.

Gidi kupitia ukurasa wake wa Facebook amesema hiyo haikuwa hatua bora zaidi ambayo Sauti Sol walipaswa kuchukua kufuatia yaliyotokea.

Mtangazaji huyo ambaye aliwahi pia kuwa mwanamuziki amependekeza kuwa badala yake bendi hiyo ingetumia fursa hiyo kujinufaisha kifedha.

"Ulikuwa wakati wa kihistoria nchini Kenya kwa mwanamke kuteuliwa kama mgombea mwenza wa kwa mgombeaji maarufu wa Urais. Bila kujali msimamo wako wa kisiasa ni jambo la kusherehekea. Sauti Sol wangeweza kuruka kwenye meli hii ya 'woman power' na kutengeneza pesa zaidi kutoka kwa mashabiki wengi zaidi wa kike," Gidi aliandika.

Kabla ya kuwa mtangazaji, Gidi alikuwa mwanamuziki katika bendi ya Gidi Gidi Maji Maji ambayo ilivuma zaidi kutokana na kibao chao 'Unbwogable'.

Kibao hicho kilitumika sana katika kampeni za aliyekuwa rais wa tatu, Mwai Kibaki ambaye alikuwa anapeperusha bendera ya Narc-Kenya.

Gidi amefichua kwa kuwa hawakupokea malipo yoyote kutoka kwa chama hicho walitumia fursa hiyo kuunda shati ambazo waliuza sana katika mikutano ya kisiasa.

"KANU ilitaka kuununua wimbo huo lakini tukakataa, haukuwa wetu tena bali ulikuwa wimbo wa Taifa wa mapambano ya watu wakati huo. Ulikuwa ni wakati UNBWOGABLE. Sauti Sol wana haki ya kudai malipo kwa ajili ya matumizi ya wimbo wao lakini ninahisi walipaswa kuifanya chini ya maji na kutumia wakati wa kuwezesha wanawake kujinufaisha kifedha," Alisema. 

Aidha mtangazaji huyo amempongeza Martha Karua kwa uteuzi wake kuwa mgombea mwenza wa Raila.