Ujumbe wa Gidi kwa Ruto baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wake

Mtangazaji huyo alibainisha kuwa sasa ni wakati wa rais mpya kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.

Muhtasari

•Gidi aliandika ujumbe wa pongezi kwa mgombea urais huyo wa Muungano wa Kenya Kwanza baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wake.

•Pia alimshukuru mgombea wa Azimio-One Kenya Raila Odinga kwa mchango wake mkubwa katika kupigania demokrasia.

Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Joseph Ogidi almaarufu Gidi amempongeza rais mteule William Ruto.

Gidi alichukua hatua ya kuandika ujumbe wa pongezi kwa mgombea urais huyo wa Muungano wa Kenya Kwanza baada ya mahakama ya Upeo kuidhinisha ushindi wake siku ya Jumatatu.

"Hongera Rais mteule William Samoei Ruto. Hongera pia wananchi wa Kenya kwa hatua tuliyopiga katika demokrasia yetu," aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliambatanisha ujumbe huo na picha yake na Ruto wakati wa mahojiano ya moja kwa moja katika makazi yake rasmi ya Karen mnamo Julai 13, 2021.

Mtangazaji huyo alibainisha kuwa wakati wa siasa umekwisha na sasa ni wakati wa rais mpya kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.

"Sasa ahadi zitimizwe, ajenda ya kiuchumi ya  Bottom up. Mungu ibariki Kenya 🙏🏿🙏🏿," alisema.

Pia alimshukuru mgombea wa Azimio-One Kenya Raila Odinga kwa mchango wake mkubwa katika kupigania demokrasia.

"Asante Baba Raila Amolo Odinga kwa mchango wako katika demokrasia yetu,"

Jumatatu adhuhuri, mahakama ya upeo kwa kauli moja ilitupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Ruto ambayo iliwasilishwa na kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na wahusika wengine.

Katika hukumu iliyosomwa na Jaji Mkuu Martha Koome, mahakama iliyaidhinisha matokeo ya urais ambayo yalitangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mnamo Agosti 15.

“Huu ni uamuzi wa pamoja. Malalamishi hayo yametupiliwa mbali, kwa hivyo tunamtangaza mlalamikiwa wa kwanza (Ruto) kuwa rais mteule,” Koome alisema.

Ruto anatarajiwa kuapishwa Jumanne, Septemba 13  na kuchukua wadhifa wa rais anayeondoka Uhuru Kenyatta.