"Inaumiza!" Gidi alalamika baada ya waandamanaji kuvamia mkahawa wa rafikiye Kisumu

Gidi alibainisha kuwa mkahawa huo hauhusiani na mwanasiasa yeyote na ukalaani shambulio hilo.

Muhtasari

•Gidi alidokeza kwamba mkahawa wa rafiki ye ulivamia baada ya kudaiwa kuwa ni wa mwanasiasa fulani.

•Alifichua kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliounga mkono wazo hilo la biashara na kusema kuwa imetengeza nafasi nyingi za ajira.

Gidi na rafikiye Silas
Image: FACEBOOK// JOE GIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Gidi ameumizwa baada ya biashara ya rafiki yake mmoja kuathirika wakati wa maandamano yaliyogeuka kuwa ghasia katika mji wa Kisumu.

Akizungumza siku ya Jumatatu, Gidi alidokeza kwamba mkahawa wa rafiki yake katika mji wa  Kisumu ulivamia na mali kuharibiwa baada ya kudaiwa kuwa ni wa mwanasiasa fulani ambaye waandamanaji walikuwa wakilenga.

Mtangazaji huyo hata hivyo alibainisha kuwa mkahawa huo hauhusiani na mwanasiasa yeyote na ukalaani shambulio hilo.

"Pitsop Kisumu haihusiani hata kidogo na mwanasiasa yeyote, inamilikiwa na wafanyibiashara vijana wenye bidii. Shambulio hilo halikufaa," alisema.

Gidi aliendelea kufichua kuwa rafiki yake alianzisha biashara hiyo kwa lengo la kuwekeza nyumbani kwao Kisumu.

Alifichua kuwa yeye ni miongoni mwa watu waliounga mkono wazo hilo la biashara na kusema kuwa imetengeza nafasi nyingi za ajira.

"Huku nikiwa sehemu ya hadithi ya Pitstop, kutoka kwa wazo, ujenzi na uzinduzi, inaumiza kuona mtu akiharibu mali kwa sababu ya uvumi,"

"Pitstop Kisumu imeajiri vijana wengi kutoka kisumu. Mfano walinzi, wapishi, wahudumu, ma-DJ na mameneja. Sio haki kuilenga tu kwa sababu ya uvumi na uwongo." Gidi alisema.

Mtangazaji huyo mahiri alimfariji rafiki huyo wake kwa hasara kubwa ambayo ilimpata baada ya uvamizi huo wa Jumatatu.

Pia alitumia fursa hiyo kuwahimiza watu kuwekeza katika maeneo yao ya nyumbani ili kutoa nafasi za kazi kwa wengine.

"Tuhamasishe watu wetu warudi kuwekeza kwenye biashara mbalimbali zinazoweza kutengeneza ajira kwa watu wetu. Pole Sana Silas na uendelee kusaidia vijana Kisumu," alisema.

Kiongozi wa Azimio, Raila Odinga alikuwa ametangaza maandamano ya umma siku ya Jumatatu kwa lengo la kushinikiza serikali ya Kenya Kwanza kushukisha gharama ya maisha ambayo imeendelea kupanda.

Maelfu ya maandamanaji haswa wafuasi wa muungano huo walijitokeza katika miji mbalimbali nchini. Hata hivyo, maandamano katika maeneo kadhaa yaligeuka kuwa machafuko baada ya baadhi ya waandamanaji kuzua ghasia ambazo ziliwapelekea maafisa wa polisi kukabiliana nao ili kutuliza hali.