"Nikirudi baada ya miaka 20 nitakuja kukusalimia" Mwanadada amwambia mpenziwe akijiandaa kuondoka Kenya

"Mimi nishamove on wezi ujao mimi naenda Canada, niache na amani," Sharon alimwambia Kelvin.

Muhtasari

•Kelvin alisema mahusiano yake ya takriban mwaka moja unusu yalisambaratika baada ya kumshutumu mpenzi wake kwa kukosa uaminifu.

•Kelvin alijaribu kumsihi mwanadada huyo asiende Canada ila maombi yake yaliangukia masikio yaliyotiwa pamba.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Kevin Ongeri kutoka Kuresoi North alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mchumba wake Sharon Korir ambaye alikosana naye mwezi Septemba mwaka jana.

Kelvin alisema mahusiano yake ya takriban mwaka moja unusu yalisambaratika baada ya kumshutumu mpenzi wake kwa kukosa uaminifu.

"Hakuwa anapokea simu na hakuna siku aliwahi kukosa kushika. Nilimpigia saa tano nikamuuliza kama alikuwa na mwanaume mwingine hapo. Kwa hasira nikamtusi na nikamwambia akae na mwanaume huyo. Hata yeye akakasirika," alisimulia.

Kelvin aliendelea, "Hata mimi nikikosa kushika simu alikuwa ananisomea. Labda nilimchukulia vibaya. Ningependa kuomba msahama kwa jinsi nilimtusi. Tulizungumza nikamuomba msamaha lakini hakusema chochote. Tangu tukosane hatujaonana tena."

Kelvin alidai kwamba tayari alikuwa amemtambulisha mpenziwe huyo kwa wazazi wake ila hakuwa ameenda kwao.

Sharon alipopigiwa simu alisema alikasirishwa sana na matusi ya Kelvin na kuweka wazi kwamba tayari amesonga mbele na maisha yake.

"Mimi nishamove on na maisha yangu. Kulingana na alivyonitusi mimi sikufurahia," Sharon alisema.

Alisema kwamba hakuwa na ubaya wowote na Kelvin bali na matusi aliyomtupia.

Kelvin alimuomba msamaha mpenzi huyo wake wa zamani na kujitetea kwamba alimtusi kutokana na hasira.

Sharon alisema, "Mimi nishakubali msamaha lakini kurudiana na wewe siwezi. Itakuwa ngumu. Acha nitulie, nikiamua nimove on ni sawa."

Aliongeza, "Mimi nishamove on wezi ujao mimi naenda Canada, niache na amani. Acha niende nitulie huko nikipata mtu wa kunipenda ni sawa. Roho ilitoka. Sitalazimisha roho yangu kukupenda. Sikulazimisha roho yangu kukupenda, nilikupenda bure."

Kelvin alijaribu kumsihi mwanadada huyo asiende Canada ila maombi yake yaliangukia masikio yaliyotiwa pamba.

Sharon alijibu, "Nikirudi baada ya miaka 20 nitakuja kukusalimia."

Kelvin hakuwa na budi ila kukubali msimamo wa mchumba huyo wake wa zamani.