(+Video) Mungu ameumba vitu vyake sawa! Napenda kunengua kiuno, itabidi mzoee- Millicent Omanga

Muhtasari

•Mashabiki wengi walihoji kwa nini seneta huyo mteule amewekeza nguvu zake nyingi katika kucheza densi kwa mtindo maarufu kama 'twerking' badala ya kuuza sera zake tu.

•Omanga alipuuzilia mbali  madai kwamba chama chake cha UDA kinamtumia tu kutumbuiza katika mikutano ya kisiasa  lakini hakimchukulii kwa makini.

Millicent Omanga na Massawe Jappani katika studio za Radio Jambo
Millicent Omanga na Massawe Jappani katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Mwaniaji wa kiti cha mwakilishi wa wanawake katika kaunti  ya Nairobi, Millicent Omanga aikuwa mgeni wetu katika kipindi cha Bustani la Massawe siku ya Alhamisi.

Mojawapo ya mambo ambayo mashabiki wengi walituma jumbe wakimtaka azungumzie ni usakataji deni wake wakati wa mikutano ya kisiasa. Mashabiki wengi walihoji kwa nini seneta huyo mteule amewekeza nguvu zake nyingi katika kucheza densi kwa mtindo maarufu kama 'twerking' badala ya kuuza sera zake tu.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto alisema kunengua kiuno ni hobby  yake na haoni tatizo lolote kwake kufanya kile anachokipenda hata katika mikutano ya kisiasa.

"Kwa nini nisipige densi? Hobby yangu ni kusakata densi na nitacheza siku yoyote. Mimi nimependa kudensi na sijui kwa nini imekuwa vibaya Millicent Omanga akiwa kwa jukwaa akicheza densi. Ata mamangu anapenda kucheza densi. Mungu ameumba vitu vyake sawasawa, tumeumbwa kwa mfano wa Mungu," Omanga alisema

Omanga alipuuzilia mbali madai kwamba chama chake cha UDA kinamtumia tu kutumbuiza katika mikutano ya kisiasa  lakini hakimchukulii kwa makini.

Aliwaomba Wakenya wakome kuangazia tu uchezaji densi wake bali pia wazungumzie miradi ambayo ametekeleza.

"Watu watasema nipunguze vile nacheza densi. Mimi napenda kucheza  densi, itabidi wazoee," Alisema.

Baada ya kipindi, mwanasiasa huyo aliendelea kuonyesha ubabe wake katika kunengua kiuno. Tazama hapa:-