Mamangu ni pasta, hakufurahia jinsi nilivyomfokea kanjo - Gloria Ntazola

Mrembo huyo mjasiriamali wa maduka mawili ya vipodozi jijini Nairobi alifichua kwamba ana miaka 25

Muhtasari

• Mrembo huyo hata hivyo aliweka wazi kwamba hajutii kwa kile alichokifanya bali anajuta tu kwa jinsi alivyomkabili kanjo kwa lugha kali tena ya matusi.

Gloria Ntazola.
Gloria Ntazola.
Image: Instagram

Mrembo Gloria Ntazola aliyevuma baada ya kukabiliana na askari wa kaunti, maarufu Kanjo amesema kwamba licha ya watu wengi mitandaoni kumshabikia kwa kitendo hicho cha ujasiri cha kumkabili askari huyo, wazazi wake na mpenzi wake hawakufurahia hata kidogo.

Ntazola aliweka wazi kwamba mama yake ni mchungaji wa kanisa na kitendo chake kumfokea kanjo kwa ukali mithili ya simbabukaa aliyejeruhiwa hakikumfurahisha kidogo na alisema kwamba ni maadili mapya kabisa aliyoyapata mjini kinyume na yale aliyomkuza nayo.

“Mama yangu ni mchungaji, hakufurahia kabisa jinsi nilivyomkabili kanjo, alinipigia simu akiniuliza kwa nini nilikuwa hivyo lakini nikamwambia Nairobi lazima ukuwe na ngozi ngumu,” Ntazola alisema.

Alisema pia baba yake hakufurahia ya kitendo chake cha kukabiliana na kanjo lakini pia mpenzi wake naye mara ya kwanza hakufurahia lakini baadae alimpongeza kwa kumzima kanjo.

Mrembo huyo mjasiriamali wa maduka mawili ya vipodozi jijini Nairobi alifichua kwamba ana miaka 25 na katika mitandao ya kijamii yeye hufanya ni kukuza maudhui ya kuchekesha.

Mrembo huyo hata hivyo aliweka wazi kwamba hajutii kwa kile alichokifanya bali anajuta tu kwa jinsi alivyomkabili kanjo kwa lugha kali tena ya matusi.

Baada ya akaunti yake ya TikTok kuzama kwa kile anahisi ni kutokana na kutumia lugha chafu akimrekodi kanjo, Ntazola alisema hata yeye alishangazwa na jinsi mashabiki wake waliweza kujibu kwa kumfuata katika akaunti mpya.

“Akaunti yangu ilizama nafikiri ni kwa vile nilitumia lugha ya matusi dhidi ya kanjo, lakini baada ya kuwaambia watu nimeanzisha akaunti mpya nilishangazwa sana kwa jinsi walinifuata kwa haraka na kwa wingi, kwa sasa niko na wafuasi Zaidi ya elfu 50,” Ntazola alisema kwa madaha.