"Patanisho!" Mwanadada alimwacha mumewe na mtoto wa miezi 6 amvunja moyo zaidi

Caroline alipopigiwa simu alisema "Awache ujinga!" kisha akakata simu mara moja.

Muhtasari

•Protus alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika mwaka wa 2020 baada ya kumfungulia mkewe biashara, hatua iliyofanya mienendo yake ibadilike.

• Protus aliweka wazi kwamba ameridhika kwani alitaka tu kujua msimamo wa mzazi huyo mwenzake.

Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Protus Makoha (27) kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Caroline Nangila (26) ambaye alitengana naye takriban miaka mitatu iliyopita.

Protus alisema ndoa yake ya miaka miwili ilisambaratika mwaka wa 2020 baada ya kumfungulia mkewe biashara, hatua iliyofanya mienendo yake ibadilike.

"Tulikuwa tunaishi tu vizuri Mungu akatubariki nikapata kazi na nikamfungulia biashara. Baadaye akapata pesa kidogo akaanza kuingia kwenye mambo sio mazuri, akaanza kuleta madharau kwa nyumba, akiona nimenunua nguo nzuri anachoma anadhani niko na wanawake.  alianza kujipatia shughuli nyingi. Hakuwa mtulivu," Protus alisimulia.

Aliongeza, "Siku moja nilipata ameenda. Alikuwa ameanza kunishuku tu, akaenda na kuniachia watoto. Nilijaribu kumtafuta arudi tulee mtoto anasema atarudi tu. Kwa sasa Ako tu kwa kazi ya hoteli."

Caroline alipopigiwa simu alisema "Awache ujinga!" kisha akakata simu mara moja.

Hata hivyo, Protus aliweka wazi kwamba ameridhika kwani alitaka tu kujua msimamo wa mzazi huyo mwenzake.

"Mimi nilikuwa nataka tu kujua uamuzi wake. Hata kuna dadake huwa anapigia simu anamtuma kwangu akisema anataka kuniongelesha. Mimi nikimpigia simu ananiblock. Vile ameamua ni sawa tu," Protus alisema.

Protus alisisitiza kwamba mzazi huyo mwenzake amekuwa akimtafuta na kudokeza nia ya kutaka kurudiana naye.

"Mambo huenda na utaratibu. Nilikuwa nataka kuhakikisha ndio nipange mambo mengine polepole. Nimejua msimamo wake. Nimeamua nimove on. Aliacha katoto kakiwa kadogo miezi sita nimeng'ang'ana nako," alisema.

Je, ushauri wako kwa Protus ni upi?