Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya mumewe kumshuku kuwa na mpango wa kando

Muhtasari

•Alex alisema mkewe aliondoka asubuhi moja na kuondoka bila kumfahamisha alikokuwa anaenda wala sababu zake za kuondoka.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost kitengo  cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Alex Lentoi , 29, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Susan Lumacia ,27, ambaye walikosana naye katika hali tatanishi.

Alex alisema mkewe aliondoka asubuhi moja na kuondoka bila kumfahamisha alikokuwa anaenda wala sababu zake za kuondoka.

Alex hata hivyo alifichua kuwa walikuwa wamekosana hapo awali baada yake kumshuku mkewe kuwa na mpango wa kando.

"Tulikuwa tumekosana mwezi mmoja uliopita. Nilienda nyumbani kwetu kidogo. Niliporudi aliama asubuhi akaenda bila kuniambia," Alex alisimulia.

"Kuna simu alikuwa amepigiwa usiku nikamuuliza ni ya nani. Akasema ni mtu kutoka nyumbani. Nikajaribu kufuatilia nikaona ni uwongo Nilikuwa nashuku hiyo simu ni ya mpango wa kando. Alikuwa anatumiwa meseji lakini singefuatilia sana," Alisema.

Alex alifichua kuwa alimuoa mkewe tayari akiwa na mtoto mmoja kisha wakabarikiwa na mtoto mwingine pamoja.

Juhudi za kumfikia Susan ziligonga mwamba kwani tayari alikuwa amezima simu.

Alex hata hivyo alimuomba mkewe msamaha hewani na kumsihi arudi ili waweze kuendelea na mahusiano yao na kulea watoto wao.

Alisema wamekuwa wakiwasiliana ila Susan amekuwa akimpa ahadi za kurudi za uwongo.

Alex alisema licha ya yaliyotokea amekuwa akishughulikia watoto wao.