Patanisho: Mama Carol aachwa kwa kunyoa box

Muhtasari

•Mama Carol alisema aligura ndoa yake ya  miaka mitatu baada ya mumewe kulalamika kuhusu mtindo wake wa kunyoa.

•Samuel alipopigiwa simu alilalamika kuwa mtindo ambao mkewe alinyoa "Ni style ya vijana".

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Mama Carol alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Samuel Ojwang'.

Mama Carol alisema aligura ndoa yake ya  miaka mitatu baada ya mumewe kulalamika kuhusu mtindo wake wa kunyoa.

"Tulikosana juu nilinyoa box. Hakuwa anataka ninyoe box. Alikuwa anataka nisukwe nywele naye hakuwa anataka," Mama Carol alisimulia.

Mama Carol alieleza kuwa mumewe alimwelekeza abadilishe mtindo huo na akampatia sharti kuwa asinyolewe nywele yote.

Hata hivyo hakufuata agizo la mumewe na hapo akakasirika na hata kumpiga, jambo ambalo lilimsukuma kugura ndoa.

"Alikuwa anafanya kazi ya shamba. Aliporudi nikamwambia nataka kunyoa mtindo ambao nataka. Aliniambia nisinyoe kipara lakini nikanyoa akakasirika. Alinipiga nikaona siwezi kuvumilia nikatoroka," Alisema.

Mama Carol pia alifichua kuwa mumewe alikuwa na mke mwingine ambaye alidai alikuwa analeta fitina katika familia yao.

Samuel alipopigiwa simu alilalamika kuwa mtindo ambao mkewe alinyoa "Ni style ya vijana".

Hata hivyo aliahidi kuenda nyumbani kwa kina mkewe ili waweze kushiriki kikao katika juhudi za kusuluhisha mzozo wao.

"Vile alitoka pekee yake sikumfukuza. Lazima tuongee. Nitaenda kwao tuongee kama atarudi," Samuel alisema.

Je, mwanaume anafaa kuamua jinsi mkewe atajiweka?