Patanisho: Niko karibu kupata mwingine na nitampata!- Jamaa amfungukia mpenziwe mjamzito

Muhtasari

•Gakii alisema alikuwa kwenye mahusiano na jamaa huyo kutoka Bomet mpaka kufikia hatua ya kubeba ujauzito wake.

•Ng'eno alidai kuwa mwanadada huyo alianza kumshuku kuhusu mambo mbalimbali, jambo ambalo halikumpendeza.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi mwanadada aliyejitambulisha kama Lydia Gakii alituma ujumbe akiomba kusaidiwa kupata ukweli kutoka kwa mpenzi wake Josphat Ng'eno.

Gakii alisema alikuwa kwenye mahusiano na jamaa huyo kutoka Bomet mpaka kufikia hatua ya kubeba ujauzito wake.

Alieleza kuwa uhusiano wake na Ng'eno ulianza kuyumba mwezi Machi ambapo alianza kumshuku kuwa na mke mwingine.

"Niko na mimba yake. Nikimuuliza kama ana mke mwingine anasema namuuliza maswali ya Maternity. Anashughulikia mimba lakini hataki nimuulize maswali ya bibi," Gakii alisema.

Alisema kuwa mpenzi huyo wake alikuwa ameahidi kumuoa na hata kuchukua namba za simu za kakake na wazazi wake.

Mwanadada huyo hata hivyo alianza kupata hisia za kuwa amechengwa baada ya Ng'eno kuanza kuepuka simu zake.

"Nikimpigia napata ako mteja na baadae ananiambia ni shida ya network. Ako Bomet na mimi niko Meru. Hajawahi kuja tangu mwezi wa tatu. Nilipata mimba Novemba. Kama ako na bibi lazima tuachane mimba haiwezi kufanya," Alisimulia.

Ng'eno alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa tayari amechoshwa na kuwa kwenye mahusiano na Gakii.

Alifichua kuwa walijuana na Gakii kupitia simu kisha baadae akafunga safari ya kuenda kukutana naye Meru. 

"Tuliongea na yeye ikiwa wrong number mpaka siku moja nikwambia nitaenda Meru. Ilikuwa mara yangu ya kwanza," Alisema.

Ng'eno hata hivyo alidai kuwa mwanadada huyo alianza kumshuku kuhusu mambo mbalimbali, jambo ambalo halikumpendeza.

Pia alidai kuwa Gakii tayari alikuwa amemfahamisha kuwa ameavya ujauzito wa mtoto wao aliyedai amebeba tumboni.

"Hakuna cha kusema hapo. Wewe ndio ulianza hayo maneno. Umekuwa kichwa ngumu. Kila siku nakwambia. Tulimalizana na wewe juzi wakati ulinitumia ujumbe. Sipendi hiyo kudanganya kwako. Unanibeba utoto," Ng'eno alimwambia Gakii.

Aliongeza "Huwa ananishuku sana. Niko karibu kupata mke mwingine na nitampata. Mambo yake sitaki tena. Naona yeye sio mtu mzuri. Aliniambia kuwa alikuwa ananipima kuhusu mimba," 

Je, una ushauri upi kwa wawili hao.