Patanisho: Jamaa apigiwa simu na mwanaume mwingine na kuagizwa aachane na mkewe

Pamela alisisitiza kuwa kazi yake ndiyo imekuwa ikifanya ashindwe kuwasiliana na mumewe.

Muhtasari

•Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 20 alidai kuwa kwa muda mrefu mumewe amekuwa akimshtumu kwa kutoka nje ya ndoa yao ya mwaka mmoja tangu alipohamia mjini Kisumu kwa ajili ya kazi.

•Pamela alimuomba mumewe kumpatia nafasi ya mwisho na kumhakikishia kuwa atabadilisha tabia zake.

Pamela Akinyi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Evans Okoth kufuatia misukosuko iliyokumba ndoa yao. 

Mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 20 alidai kuwa kwa muda mrefu mumewe amekuwa akimshtumu kwa kutoka nje ya ndoa yao ya mwaka mmoja tangu alipohamia mjini Kisumu kwa ajili ya kazi.

"Anasema ni kama natoka nje ya ndoa na hiyo inaniumiza sana moyoni. Nilitoka kwangu mwezi Agosti. Sasa naishi na shangazi yangu Kisumu kwani nafanya kazi kwa Mpesa iliyo huku. Wakati mwingine huwa nafika kwa nyuma nikiwa nimechoka nalala mapema. Huwa nashindwa hata kujibu meseji zake. Yeye anashuku kuwa wakati mwingine huwa nalala kwa mwanaume mwingine," Pamela alisema.

Alisisitiza kuwa kazi yake ndiyo imekuwa ikifanya ashindwe kuwasiliana na mumewe mara kwa mara na kubainisha kuwa hajawahi kuwa na mahusiano ya kando.

Evans alipopigiwa simu alisema kuwa mienendo yenye utata ya mke wake ndiyo imekuwa ikifanya amtilie shaka.

"Majibu yake huwa hayanifurahishi. Nikipiga simu huwa anakata. Nikipiga tena napata yuko busy," alisema.

Aliongeza, "Nishafanya maamuzi yangu. Nilimwambia vizuri kuwa mambo ambayo amenifanyia ni mingi nataka kuishi maisha yangu," 

Evans alifichua kuwa amewahi kupigiwa simu na mwanaume mwingine na kuagizwa aachane na mkewe.

"Hata wewe unaweza kufurahia mwanaume mwingine akinipigia simu na kuniambia ati niachane na mke ambaye nishaoa?" alihoji Evans.

Pamela alidai kuwa hana uhusiano wowote na mwanaume aliyempigia mumewe na kusisitiza kuwa amekuwa mwaminifu kwake.

"Tusameheane na turudiane.  Mimi simjui huyo mtu," alisema.

"Nakupenda na hakuna mtu mwingine. Wewe unafikiria vitu haziko. Hakuna chenye nafanya mbaya"

Evans alisema, "Mimi sipendi kudanganywa. Huyo msichana ni muongo. Nimechoka kuvunjika moyo mara nyingi. Sina shida na yeye, nataka awe mtu mkweli. Akibadilika itakuwa sawa."

Pamela alimuomba mumewe kumpatia nafasi ya mwisho na kumhakikishia kuwa atabadilisha tabia zake.

"Kwanzia leo nitabadilika. Hata kama ni mambo ya simu nitakuwa napokea. Nitaacha kuongea na watu wengine, nitakuwa na wewe pekee. Nipatie nafasi ya mwisho," aliomba.

Evans alikubali kumsamehe mkewe na kumuomba kutimiza ahadi aliyotoa hewani.

Gidi alimshauri Pamela kutomkosea mumewe hasa kwa kuona jinsi alivyo muvumilivu.

"Ukipata mwanaume ambaye anakuvumilia, shikilia tafadhali. Usikuwe na mbio. Akikupigia simu sio ati ukate,"