Patanisho: Mume wangu amewahi kunishikia panga mara tatu

Sheila alisema mumewe amekuwa akitenda makosa ikiwemo kuenda nje ya ndoa bila kuonyesha majuto.

Muhtasari

•Sheila alifichua kuwa hakujakuwa na amani katika ndoa yake kwa miaka mitatu kati ya minne ambayo wamekuwa pamoja.

•Aliongeza, "Mimi sasa nataka kutoka. Amewahi kunishikia panga mara tatu!" 

Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Sheila Kosgei (26) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Edward Maiyo (46) ambaye hajawa na uhusiano mzuri naye.

Sheila alifichua kuwa hakujakuwa na amani katika ndoa yake kwa miaka mitatu kati ya minne ambayo wamekuwa pamoja.

"Tumekuwa tukizozana na yeye kila wakati. Mwaka moja pekee ndio tulikuwa sawa. Miaka hiyo ingine tumekuwa tukizozana," alisema.

Alidokeza kuwa mumewe amekuwa akitenda makosa ikiwemo kuenda nje ya ndoa bila kuonyesha majuto yoyote.

"Wakati mwingine anaweza kuwa na mwanamke huko nje. Nikimuuliza badala aombe msamaha anaanzaa kunitusi tu. Miaka mitatu ambayo imepita tumekuwa tukizozana tu. Mimi sijawahi kumkosea," alisema.

Alisema kuwa amekuwa akitia juhudi kubwa kuleta amani katika ndoa yao ila juhudi zake hazijawahi kuzaa matunda.

"Huwa anabadilika wiki moja alafu wiki nyingine anaanza maneno," alisema.

Aliongeza, "Mimi sasa nataka kutoka. Amewahi kunishikia panga mara tatu!

Sheila hata hivyo alikiri kuwa anahofia kugura ndoa yake kwa sababu ya afya ya mwanawe ambaye huathirika akitoka katika mazingira yale.

"Kuna siku tulikosana naye nikaenda nyumbani na mtoto mmoja. Nilipofika kule aliugua nikaamua kurudi.  Naskia vibaya kuacha mtoto wangu,

Juhudi za kumsaidia Bi Sheila ziligonga mwamba kwani Bw Maiyo alikosa kushika simu licha ya Gidi kufanya majaribio kadhaa.