Patanisho: Jamaa amuoa rafiki ya mkewe baada ya kuachwa

Jerotich alifichua kuwa mke huyo wa pili wa mumewe alikuwa rafiki yake wa karibu.

Muhtasari

•Jerotich alisema aligura ndoa yake ya miaka 19 na kuchukua watoto wake watatu pamoja naye kufuatia tabia ya vurugu na uhanyaji ya mumewe.

•Bungei alitetea ndoa yake mpya na rafiki ya Jerotich na kudokeza kuwa anafurahia kujenga familia naye.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Stella Jerotich kutoka Uasin Gishu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Daniel Bungei ambaye alitengana naye miaka miwili iliyopita.

Jerotich alisema aligura ndoa yake ya miaka 19 na kuchukua watoto wake watatu pamoja naye kufuatia tabia ya vurugu na uhanyaji ya mumewe.

"Alikuwa akinipiga tangu anioe. Nilijaribu kuvumilia kwa sababu ya watoto," alisema.

Alidokeza kuwa baada ya kugura ndoa yake, Bw Bungei alimchukua mwanamke aliyekuwa mpango wake wa kando kuwa mke wake.

"Mwezi wa tatu, walikuja tukawa na kikao na wazee. Kumbe alikuwa na mpango wa kuoa mpango wa kando!" alilalamika.

Aliongeza, "Lakini mke mwingine, sio shida kwangu!" 

Jerotich alifichua kuwa mke huyo wa pili wa mumewe alikuwa rafiki yake wa karibu.

"Huyo mama ako na watoto wawili wake, alikuwa rafiki wangu. Nilikuwa naenda kwake naye anakuja kwangu,"

"Alipata watoto naye tukiwa kwa ndoa. Nilikuwa nimekubali. Hapo awali alikuwa amesema hawezi kumuoa,"

Alisema mumewe alikuwa amefanya juhudi za kufufua ndoa yao ila haikuwezekana kutokana na masuala ya kifamilia.

"Nilikubali kurudi, lakini kulikuwa na masuala ya familia. Alisema nimalize hayo mambo ili nirudi. Kabla nirudi akaoa huyo msichana. Sina shida na mke wake, huyo ni wake sio wangu," alisema Jerotich.

Bw Bungei alielezea kufadhaika kwake kutokana na majaribio yake mengi ya hapo awali yaliyofeli ya kurudiana na mkewe.

Alisikika mwenye kinyongo kikubwa na Jerotich na familia yao na kuonyesha wazi kuwa tayari ameshasonga mbele na maisha yake.

"Mwingine ashaingia.Nikusamehe kwa nini na unajua niko na bibi mwingine hapa? Si uko kwako," alimuuliza Jerotich.

Bungei alifichua kuwa wazazi wa Jerotich waliweka wazi kuwa hawataki binti yao arudi katika ndoa yao.

"Nimewapeleka majirani wangu wote na ndugu zangu  kwao hata wameniambia wamechoka. Anakuja siku mbili alafu anatoka," alisema.

"Aliambia wazazi wake eti nataka kumuua. Ashanunuliwa shamba na kujenga kwake. Wazazi wake walisema mtoto wao anateseka. Amenizungusha sana mpaka nikaona nitafute mwingine," alisema.

Bungei alitetea ndoa yake mpya na rafiki ya Jerotich na kudokeza kuwa anafurahia kujenga familia naye.

"Hata kama ni rafiki yake, si afadhali nimchukue kuliko nihangaike!" alisema.

"Mama yako alisema mtoto wao ameteseka sana mpaka ndugu zako wakachanga pesa wakakununulia shamba. Unataka ukuje huku tena ukufe na stress?" Bungei alimlalamikia mzazi huyo mwenzake.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziligonga mwamba kwani Bungei alionyesha wazi kwamba hakuwa tayari kumchukua tena mkewe.

"Acha nichunge watoto, kurudiana itakuwa ngumu!" Bungei alisema

Jerotich alisema ,"Ni sawa, Nimekubali. Mimi bado namtambua kama mume wangu na baba ya watoto wangu. Na awalipie watoto wake karo."

"Najua mimi ndio mke mkubwa. Akae akijua ako na wake wawili na watoto sita. Mimi ndio mkubwa, yule ako kwa nyumba ni mdogo!" aliongeza.

Bungei hata hivyo alionyesha waziwazi kuwa hayupo na nia ya kurudiana na mwanadada huyo htata katika siku za usoni.

"Gidi, hiyo ni ndoto!" alisema.