Patanisho: "Tafuta baba ya mtoto uende uolewe, mimi sio babake!" Jamaa amruka mwanawe hewani

"Mtoto anafanana na Dan na mama yake!" Mercy alisema.

Muhtasari

•Mercy alifichua kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilivunjika wakati mumewe alipomfukuza kwa sababu ya ulevi. 

•Dan alidai kuwa mtoto wa mpenzi huyo wake wa zamani sio wake na kumwagiza atafute baba yake halisi .

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mercy Betinga ,23,  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Duncan Omari ,25, ambaye alitengana naye mnamo Julai mwaka jana.

Mercy alifichua kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilivunjika wakati mumewe alipomfukuza kwa sababu ya ulevi. 

"Nilikuwa nimekasirika kidogo nikakunywa pombe. Kabla ya kuoana tulikuwa tunakunywa sote. Wakati tulipooana tulikubaliana kuacha," alisema.

Alieleza kuwa alianguka kwenye mtego wa kubugia kileo licha ya makubaliano ya awali baada ya kukutana na marafiki zake.

"Alikasirika akaniambia niende, nikaondoka. Nilienda nyumbani alafu baadae nikakuja mahali naishi sasa," alisema.

Mercy alisema huwa anawasiliana na Dan mara kwa mara ila mazungumzo yao hayajakuwa mazuri kila wakati.

Pia alifichua kuwa mume huyo wake wa zamani tayari amepata mke mwingine, jambo ambalo anafahamu vizuri.

 "Tayari amepata mtu. Lakini nataka tu kurudi nyumbani. Mimi ndio mke mkubwa. Najua bado ananipenda nami nampenda," alisema.

Alidai kuwa tayari ameacha kunywa pombe.

Duncan alipopigiwa simu alithibitisha kuwa tayari amesonga mbele na maisha yake. Aliweka wazi kwamba hana nia ya kurudiana na Mercy.

"Msamaha kwa sasa ni ngumu. Nilishamove on kitambo. Saa hii niko  na bibi na mtoto. Huwezi kuenda mwaka moja alafu useme unataka turudiana. Wewe songa mbele na maisha yako," Dan alimwambia Mercy.

Pia alidai kuwa mtoto wa mpenzi huyo wake wa zamani sio wake na kumwagiza atafute baba yake halisi .

"Tafuta baba ya mtoto uende uolewe, mimi sio baba yake. Usijaribu kunikwamia kwa sababu unajua nyumbani. Mtoto si wangu,"

Alisema "Huyo mwanadada amechanganyika. Wakati alipokuja nyumbani alikuwa na watu wengi sana. Alitembea sana ndio akakuja kwangu. Tulikuwa pamoja wakati alipopata mtoto. Tulikaa sana na yeye ndio maana huenda tufanana na mtoto."

Mercy kwa upande wake alisisitiza kuwa mtoto ni wa Duncan na kumtaka awajibike katika malezi.

"Anafanana na Dan na mama yake!" alisema.

Duncan aliweka wazi kwamba Mercy alikuwa na muda mwingi wa kumtafuta hapo awali na kudai alianza tu baada ya kupata taarifa kuwa amepata mke mwingine.

"Mimi niko na mtoto wangu. Wakati huo wote angekuwa amekuja nyumbani. Vile amejua nimeoa ndio ameanza kunipigia simu. Niliwahi kumpata na bwana na sikumuuliza," alisema.

"Aachane na mimi, mabwana ni wengi," aliongeza.