Patanisho: Mama awafukuza wake wawili wa mwanawe, aachiwa watoto watano kulea

Jairus alifichua kuwa mkewe aliolewa na jirani wake baada ya kukosa mahali pa kwenda.

Muhtasari

•Jairus alidai kuwa uhusiano wake na mzazi huyo wake umedorora baada ya kuwafukuza wake zake wawili.

•Jairus alisema alisikitika sana baada ya mama yake kuvunja ndoa zake na ndiposa akagura na kumwachia watoto.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost, kitengo cha Patanisho, Jairus alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake Bi Hannah.

Jairus alidai kuwa uhusiano wake na mzazi huyo wake umedorora baada ya kuwafukuza wake zake wawili.

"Baba alikufa 2004. Nilipata bibi. Nilikuwa nikimsaidia mama nyumbani pamoja na familia yangu. Vile mama aliona nimeanza kushindwa kumsaidia, alimfurusha mke wangu. Alienda akaniachia watoto watatu, mapacha na mwingine mmoja," Jirus alisimulia.

Aliongeza "Baada ya mwaka mmoja nilioa mke wa pili. Tulikaa na yeye kwa ndoa kwa miaka mitatu na tukabarikiwa mapacha wawili.  Nilikuwa kazini wakati mama alimfukuza na akaacha watoto." 

Jairus alifichua kuwa mkewe wa kwanza aliolewa na jirani wake baada ya kukosa mahali kwa kwenda. Alisema juhudi zake zote za kumrejesha nyumbani ziliangulia patupu.

Alisema kuwa sasa amekaa miaka miwili bila mke baada ya mama yake kuwafurusha wawili wa kwanza.

"Nimejaribu kumwongelesha mama, ananipeleka mbio. Watu wa ukoo pia wanaogopa kuenda karibu naye. Huwezi kaa na yeye dakika mbili mkapiga stori.. Ningependa kuomba msamaha angalau anipatie uhuru wa kuoa."

Bi Hannah alipopigiwa simu alipuuzilia mbali madai ya kuwafukuza wake za mwanawe na kuweka wazi kwamba hataki kuzungumza naye.

"Sina la kuongea na yeye sasa. Itakuwaje nimewafukuza mabibi zake na ameniachia watoto wake watano nawashughulikia. Yeye hashughuliki. Siongei kwa radio. Wacha akae, na mimi nikae," alisema kabla ya kukata simu.

Jairus alisema alisikitika sana baada ya mama yake kuvunja ndoa zake mbili na ndiposa akagura nyumbani na kumwachia watoto.

"Nilikuwa nasaidia mama na watoto. Vile nilipata kazi nikaenda nikamwachia mama."

Bi Hannah alipopigiwa simu mara ya pili alisema, "Mimi naumia na watoto. Naweza kubali vipi kuwafukuza mabibi wake na ameniachia watoto watano? Mimi nilikuwa kwa soko nikapata bibi yake ameenda.

Alimwagiza mwanawe afike nyumbani ili achukue watoto wake akidai kwamba yeye mwenyewe amechoka.

"Akuje achukue watoto wake aende nao, mimi simtaki na sitaki watoto wake"

Jairus hakuwa na budi ila kukubali agizo la mamake. Alisema kuwa ataenda nyumbani hivi karibuni na kuwachukua wanawe.