Patanisho: Mwanajeshi aachwa kwa kukosa kununua nguo za sikukuu, mkewe amwambia apeleke pesa kwa warembo

Mutua alisema mkewe hakufurahishwa na yeye kukosa kumtumia pesa na kufuatia hilo akamtusi.

Muhtasari

• Mkewe alisema kuwa mke wake alikasirika na kujitenga naye baada ya kukosa kumtumia pesa za kununua nguo za sikukuu kama walivyokuwa wamekubaliana hapo awali.

•Mutua alisema hajaweza kuonana na mkewe tangu alipoenda nyumbani kwao mwezi uliopita licha ya kuwa tayari amerejea jijini.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Meshack Mutua (29) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke  wake Frida Kibahara (28) ambaye alizozana naye mwezi uliopita.

Mutua ambaye alidai kuwa yeye ni mwanajeshi wa KDF alisema kuwa mke wake alikasirika na kujitenga naye baada ya kukosa kumtumia pesa za kununua nguo za sikukuu kama walivyokuwa wamekubaliana hapo awali.

"Nilifaa kumtumia shilingi 2000 za nguo mnamo Desemba 17. Ikawa sina pesa. Wakati huo alikuwa ameenda shughuli fulani kwao Meru," Mutua alisimulia.

Mwajeshi huyo alisema Fridah hakufurahishwa na hatua ya yeye kukosa kumtumia pesa na kufuatia hilo akamtusi.

"Nilipomwambia kwamba sina pesa, alisema hiyo pesa nipeleke kwa makahaba. Jana nilimtumia ujumbe kwa simu nikaona bado hajabadilisha msimamo, anasema nipeleke pesa kwa warembo," aliongeza.

Mutua alisema hajaweza kuonana na mkewe tangu alipoenda nyumbani kwao mwezi uliopita licha ya kuwa tayari amerejea jijini.

"Huwa hatuishi pamoja. Anafanya kazi mbali kutoka mahali naishi lakini huwa namtembelea," alisema.

Fridah alipopigiwa simu alikuwa mchache wa maneno. Alimwagiza Mutua ampigie simu mwenyewe kisha akakata.

Mutua hata hivyo alidokeza kuwa tayari alikuwa amechukua hatua ya kumfikia kwa njia ya simu ila mazungumzo yao hayakuwa mazuri kwani mkewe alikuwa akimtupia cheche za maneno kwa njia ya sms.