Patanisho: Mwanamume alia mkewe kutoroka na kumuachia mtoto aliyemuoa naye

Patrick alimuoa Rose akiwa na mtoto, Rose akatoroka na kuolewa kwingine akimwachia Patrick mtoto huyo.

Muhtasari

• Rose alikuja kugundua mumewe mpya Patrick alikuwa na uhusiano wa damu na mume wa kwanza aliyezaa naye kwa jina Kevo.

• Hapo ndio aliamua kutoroka na kuolewa na mwanamume mwingine kwa jina Ian kutoka Butere.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Alhamisi Januari 26 katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye kituo cha redio Jambo, mwanamume mmoja kwa jina Patrick aliwasilisha kesi ya kutaka kupatanishwa na mke wake ambaye alitoroka baada ya kuoana kwa mwaka mmoja na nusu.

Patrick alielezea watangazaji Gidi na Ghost kuwa mke wake Rose Musungu alikuja na mtoto na walikaa kwa mwana mmoja unusu katika eneo la Kiambu, lakini Desemba iliyopita, alimtaarifu mumewe Patrick kuwa alikuwa na rafiki yake Nairobi ambaye alitaka kumtembelea.

Kipindi hicho, Patrick na mkewe Rose walikuwa wamepanga kuenda kwao nyumbani ili kumtambulisha kwa watu wa kwao kama mke wake.

Patrick alimruhusu kuenda Nairobi lakini akamtaka kurejea ili waendelee na mipango mingine ya kutambulishwa kwao. Kipindi anaondoka, alimuachia Patrick mtoto wake ambaye alimuoa naye.

“Nilikuwa nimeoa mke na tulikaa kwa mwaka mmoja na nusu, Kiambu. Alikuja na mtoto kutoka Magharibi tukakaa naye. Ikafikia wakati tunaenda nyumbani kuona wazazi. Akasema ako na rafiki Nairobi kumtembelea. Alipoenda Nairobi baada ya siku mbili simu ikawa mteja.”

Rose alipochelewa kurudi, Patrick aliamua kufunga safari kwenda kwao akiwa na yule mtoto wa kambo na baada ya siku mbili ndio alipokea simu Rose akimwambia kuwa simu ilipotea. Namba aliyopiga nayo ikawa inamchanganya Patrick ambaye baadae aligundua ni ya mwanamume mwingine.

“Nikachukua mtoto nikakuja nyumbani kwetu, akaja akanipigia na namba nyingine akasema simu ilipote. Baada ya siku 2 nikapiga hiyo namba nikapata ni mwanamume akaniambia kaa ukijua ni mke wangu. Hajai shughulika kudai mtoto wake. Mtoto ako kwa mama yangu,” Patrick alielezea kwa uchungu.

Ian ambaye ni mume mpya kutoka Butere alisema Patrick hakuwa amemuoa Rose bali alikuwa anamtumia tu, alizidi kuelezea kuwa Rose ndiye alikuwa anamtumia pesa Patrick.

“Rose pahali alizaa, ako na ukoo na huyo Patrick kwa hiyo hakuna vile wanaweza kuoana,” Ian wa Butere alisema.

Kwa upande wa Rose, alimwambia Patrick kuwa ameoleka na kuondoka kwake hakutaka kumuambia moja kwa moja, kuwa aligundua baadae kuwa Patrick alikuwa na ukoo na baba wa mtoto wake – Kevo.

“Kama singekuwa na mtoto na Kevo, ningerudi kuolewa na wewe lakini sasa nimegundua wewe na Kevo ambaye ni baba watoto wangu ni binamu wako. Haiwezi kuwa,” Rose alielezea sababu yake ya kumtema Patrick.

Rose alisema hakukosewa na Patrick bali ni aibu tu ya kugundua baba wa watoto wake ana uhusiano wa damu naye.