Patanisho: Babangu alisema nalala na mamangu wa kambo

Bw Geoffrey alifichua kwamba mwanawe alikataa masomo na kuamua kwenda kuajiriwa.

Muhtasari

•Daniel alisema ugomvi baina yao ulitimbuka Machi mwaka jana baada ya mzazi huyo wake kukataa kumlipia karo ya shule.

•Daniel aliweka wazi kwamba hajui mahali mama yake halisi aliko.

•Bw Geoffrey alitupilia mbali madai ya mwanawe kuwa alimshtumu kwa kulala na mke wake.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Daniel Omoding ,18, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na babake mzazi, Geoffrey Okware ambaye alikosana naye mwaka jana.

Daniel alisema ugomvi baina yao ulitimbuka Machi mwaka jana baada ya mzazi huyo wake kukataa kumlipia karo ya shule.

"Nilikuwa sijakaa na yeye. Nilikuwa nikiishi na nyanya. Baba alitaka tuende kazi ya mjengo na yeye ndio anilipie karo. Nilikuwa na miaka 17," alisema.

Kijana huyo alieleza kwamba baada ya kukataa kuenda kazi na babake aliamua kuandamana na mamake wa kambo kuenda kibarua.

"Nilienda na mama wa kambo kibarua ya kulima ndio nipate pesa. Tulikuwa tumekosana na baba kwa sababu alikuwa amekataa kunilipia karo,"

Daniel aliweka wazi kwamba hajui mahali mama yake halisi aliko

"Tulikosana na yeye nikatoka nikaenda njia zangu. Nilirudi nyumbani hivi majuzi. Sasa naishi kwa jirani. Amekataa nikae na yeye. Anasema nitafute nyumba nikae kivyangu. Mama wa kambo pia  alitoka juzi akaenda," alisema.

Bw Geoffrey alipopigiwa simu alifichua kwamba mwanawe alikataa masomo na kuamua kwenda kuajiriwa.

"Huyo mtoto ni mjinga sana. Nilimwambia aende shule akakataa akaenda kazi ya kuchunga ng'ombe. Niliachilia yeye akaenda. Nikamwambia anisaidie na mia tatu pekee akakataa. Alienda mwaka jana na  amekuja Disemba kama hana chochote. Amekuja bure. Anatarajia mimi nimlishe na nimlipie nyumba," Bw Geoffrey alisema.

Bw Geoffrey pia alitupilia mbali madai ya mwanawe kuwa alimshtumu kwa kulala na mke wake.

"Bosi wake aliniambia ati aliacha kazi mwezi wa sita akasema anaenda kumzika nyanyake. Nyanyake aliaga miaka mitatu iliyopita sijui alikuwa anaenda kumzika gogo wapi.  Angeskia maneno yangu hangekuwa vile ako saa hii," alisema.

Babake Daniel hata hivyo alikubali kumsamehe na kukubali kuwa na kikao naye baadaye siku ya leo Jumatatu.

"Nimekusamehe lakini naomba ubadilike. Urekebishe," alisema.

Daniel pia aliweka wazi kwamba hana kinyongo na mzazi huyo wake na akaahidi kurekebisha tabia zake.