Patanisho: Baba mkwe achimbia jamaa kaburi la kumzika baada ya kumtusi

"Mzee alisema amechimba kaburi ya kunizika kwa shamba la kahawa. Niliogopa kuenda huko," alisema

Muhtasari

•Dennis, 37, alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika baada ya kuzozana na mkewe kuhusu suala la masomo ya mtoto wake wa kambo.

•Mamake Jane alifichua kwamba bintiye alikatiza ndoa na jamaa huyo kutokana na madharau mengi aliyomuonyesha.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Bw Dennis alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake wa pili Bi Sharon ambaye alimtema mwaka jana.

Dennis, 37, alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika baada ya kuzozana na mkewe kuhusu suala la masomo ya mtoto wake wa kambo.

"Tulioana naye mwaka wa 2020. Alikuwa ananidanganya eti ako na mtoto mmoja msichana. Tulikuwa tumeenda kwao, kufika nyumbani nikagundua ako na watoto wawili, msichana na mvulana. Nilikuwa nadhani ako na mtoto mmoja," alisema. 

Alisema baada ya kutembea wakwe zake, walikabidhiwa mtoto mmoja wa Jane waende naye ili aanze shule.

"Shule ilipokaribia kuanza mtoto alisema anataka kuenda kusomea kwa nyanya yake . Mama mkwe pia alisema anataka aende huko. Nilishindwa kwani walikuwa wananipima waone kama nitaweza kumshughulika," alisema.

Dennis alisema kuwa wakati alipowasiliana na mama mkwe baadaye alifahamishwa kwamba mke wake alikuwa na mpango wa kwenda Saudi Arabia, jambo ambalo hakutaka litokee kwa kuwa alitaka warudiane.

"Mke wa kwanza alikuwa wa kisirani alikuwa anatoroka miaka miwili alafu anarudi. Ndio maana nikaoa wa pili . Huyu wa pili ndiye niliona ako na heshima. Ningependa turudiane," Alisema.

Gidi alimpigia simu mamake Jane kwani Bw Dennis alidai kuwa mke huyo wake wa pili alikuwa amepoteza simu yake.

Mamake Jane alifichua kwamba bintiye alikatiza ndoa na jamaa huyo kutokana na madharau mengi aliyomuonyesha.

"Huyo waliachana na yeye, sijui anataka nini. Madharau ambayo alimfanyia hawezi kufaulu kamwe. Yeye ako na bibi na watoto. Alitaka Jane awe bibi wa pili lakini madharau alimfanyia hawezi kurudi," alisema.

Mamake Jane alisema mkwe huyo wake wa zamani alimkosea adabu babake Jane akimwambia kuwa binti huyo wake alizaliwa nje ya ndoa.

"Alidharau mzee wangu akimwambia kwamba pia yeye alizaliwa watoto kutoka nje. Aliambia mzee eti Jane alizaliwa nje," alisema.

Dennis hata hivyo alitupilia mbali madai hayo huku akidai kwamba babake Jane alikuwa amemtishia. 

"Mzee alisema amechimba kaburi ya kunizika huku kwa kahawa. Niliogopa kuenda huko," alisema.

Alimuomba mamake Jane kukubali ombi lake la msamaha ili aweze kufika nyumbani kwao ili waweze kutatua mzozo.

Mamake Jane hata hivyo aliweka wazi kuwa hakuna nafasi ya msamaha huku akifichua kwamba bintiye tayari ameenda Qatar.

"Watu wengine wanataka mtoto wewe hutaki. Ulitaka watoto wengine walale chini lakini wake alale juu. Jane alienda Qatar, tutaenda kumtoa huko?," alisema.

Aliongeza, "Ata babake hawezi kubali Jane arudi kwa Dennis." 

Mamake Jane alimtaka Dennis amsahau bintiye kabisa pamoja na familia yao yote.