Patanisho: Ataka kupatanishwa na mke aliyemuacha miaka 3 iliyopita baada ya kuchumbiana mwaka moja

Ben alisema janga la Covid-19 lilipelekea kuvunjika kwa ndoa yake.

Muhtasari

•Ben alisema ndoa yake ya mwaka mmoja unusu ilivunjika takriban miaka mitatu iliyopita baada ya kotofautiana na mkewe.

• Ben alisema kuwa bado anampenda mzazi huyo mwenzake na kumsihi warudiane ili waweze kulea mtoto wao pamoja.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Kwenye kitengo cha Patanisho, Ben Akibaya ,28, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Mama Trizah (24).

Ben alisema ndoa yake ya mwaka mmoja unusu ilivunjika takriban miaka mitatu iliyopita baada ya kotofautiana na mkewe. Kabla ya kutengana, wawili hao walikuwa wamebarikiwa na mtoto mmoja pamoja.

"Huwa tunaongea lakini hatupatani vizuri. Nikimwambia arudi anasema ningoje kidogo," Ben alisema.

Ben alisema kwamba janga la Covid-19 ambalo lilikumba dunia mwaka wa 2020 lilipelekea ndoa yake kuvunjika.

"Wakati Covid ilikuja kazi iliishi. Ilibidi tuende nyumbani. Hakutaka kukaa kwetu akaenda kwao. Wakati huo alikuwa mjamzito. Alisema anataka kuishi na mama yake mzazi. Lakini nilikuwa nashughulikia mahitaji," alisema.

Ben alisema kwa sasa mkewe huyo wa zamani anafanya kazi jijini Nairobi na anaiishi na ndugu yake.

"Hana mtoto mwingine, ni wangu tu. Huwa namshughulikia mtoto kupitia kwa nyanya yake," alisema.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziligonga mwamba kwani Mama Trizah hakukubali kuzungumza kwenye simu.

Ben alisema kuwa bado anampenda mzazi huyo mwenzake na kumsihi warudiane ili waweze kulea mtoto wao pamoja.

"Ningependa kumwambia nataka kujua msimamo wake. Nilikuwa nampenda. Akuje tulee mtoto. Akipata bwana mwingine atamtesa," alisema.

Gidi alitilia shaka hali ya uhusiano wa wawili hao akibainisha kuwa walichumbiana kwa muda mfupi kuliko ambao wametengana.