Patanisho: Jamaa awapa wasichana malazi, akana kumpa ujauzito mmoja wao akidai alisaidia tu

Christopher alidai msichana aliyesaidia alimtongoza kwa simu baada ya kufika nyumbani kwao.

Muhtasari

•Christopher alisema uhusiano wake na mkewe uliathirika baada ya msichana ambaye alikuwa amesaidia kumuomba amuoe.

•Nancy alisema alikuja kujua kuhusu msichana huyo mjamzito aliyekuwa akiishi na mumewe kutoka kwa majirani.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost Asubuhi, Christopher Oduor (24) kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Nancy Auma (22) ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.

Christopher alisema uhusiano wake na mkewe uliathirika baada ya msichana ambaye alikuwa amesaidia kumuomba amuoe.

"Nilikuja Nairobi mwezi wa nane. Mwezi Desemba nikapatana na msichana akaniomba usaidizi. Aliomba nimsaidie nauli aende kwao. Nikamwambia labda akae kwangu nikipata nauli nitampatia. Kumbe alikuwa na mimba, sikujua. Nilipata nauli baada ya wiki moja. Nilimpatia akaenda kwao," alisimulia.

Christopher alisema msichana huyo aliyesaidia alianza kumtongoza kwa simu baada ya kufika nyumbani kwao.

"Vile alienda nyumbani alianza kutuma meseji kwa simu yangu. Alikuwa anauliza kama anaweza kuja awe bibi yangu. Nikasema hapana. Wakati msichana alienda nilitumia bibi nauli akakuja, hapo ndo aliona meseji," alisema.

"Msichana huyo alikuwa analala kwa kitanda changu kwa sababu nilikuwa bize sana mchana na usiku,"

Jamaa huyo alieleza kwamba ndoa yake ya miaka miwili ilitatizika baada ya mkewe kuona jumbe za msichana huyo.

"Tunaishi na yeye lakini hatuelewani vizuri," alisema.

Nancy alipopigiwa simu alifichua kuwa mumewe alikuwa na tabia kuweka wasichana nyumbani kwa madai kwamba anawasaidia.

"Huyo alikuwa ni msichana wa pili. Alikuwa ananipigia ati mara amepata msichana mwingine ati anateseka akaamua kumsaidia. Wakati mmoja alinitumia meseji akasema kwa kuwa  yeye ndiye anatoa kila kitu nitakaa na huyo msichana cha lazima," Nancy alisimulia.

"Ilifaa nikuje Nairobi mwezi wa kumi na moja. Alikuwa ananitumia pesa za matumizi nyumbani, aliniambia pesa ambazo amenitumia naweza kuenda nayo kwetu. Nilijifanya sikuskia nikanyamaza tu," aliongeza.

Nancy alisema alikuja kujua kuhusu msichana huyo mjamzito aliyekuwa akiishi na mumewe kutoka kwa majirani.

"Kumuuliza akanipigia. Nilimwambia anitumie namba ya huyo msichana ili tuzungumze naye na akanitumia. Nikimuuliza kuhusu mimba ya msichana huyo alikuwa ananitusi na kuniongelesha vibaya. Niliachana naye tu," alisema.

Huku akijitetea, Christopher alimuomba msamaha mkewe na kuahidi kurekebisha tabia zake.

"Najua nimekukosea. Naomba msamaha. Sitaendelea na mambo hayo tena. Sitawahi kusaidia mtu kama sijakwambia. Hiyo mimba alienda nayo si yangu. Nancy mimi nimewacha ukora, nakupenda sana," alimwambia mkewe.

Nancy alikubali kumsamehe mumewe ila kwa shingo upande.