Patanisho: Jamaa ampiga mkewe baada ya kumpata akiongea na mwanaume aliyekuwa akimmezea mate

Musyoka aliahidi kutomgombanisha wala kumpiga mkewe tena.

Muhtasari

•Musyoka alifichua kuwa mkewe aligura ndoa yao ya miezi kadhaa baada ya kumgombanisha kwa kuzungumza na jamaa aliyekuwa akimfuatilia.

•Musyoka alisema baada ya mkewe kuenda wamekuwa wakizungumza na akaahidi kurudi ila bado hajachukua hatua ya kurudi.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Joseph Musyoka kutoka Kitui alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mary Birundi ambaye alikosana naye mwezi Februari.

Musyoka alifichua kuwa mkewe aligura ndoa yao ya miezi kadhaa baada ya kumgombanisha kwa kuzungumza na jamaa aliyekuwa akimfuatilia.

"Nilikuwa likizo, kuna rafiki yake msichana alikuwa anakuja kwa nyumba. Alikuwa anakuja wanatoka wanaenda. Nikamwambia hiyo tabia sio nzuri," alisimulia.

"Kuna jamaa alikuwa anamfuata fuata bibi yangu. Siku moja bibi yangu alitoka na rafiki yake wakaenda kwake nikawafuata. Karibu na kwa huyo msichana huyo, nilipata jamaa amesimama kwa barabara na wao wamesimama kwa roshani wanaongea. Nikaingia kwa hiyo ploti nikamgombanisha bibi yangu. Baada ya hapo alirudi kwa nyumba nikamgombanisha sana akatoka akaenda," aliongeza.

Musyoka alisema baada ya mkewe kuenda wamekuwa wakizungumza na akaahidi kurudi ila bado hajachukua hatua ya kurudi.

"Nilikuwa nataka nimuombe msamaha nimwambie kwamba nimeacha mambo ya kumchapa na kumgombanisha. Nimejaribu kuongea na mamake akasema hana shida atarudi." Musyoka alisema.

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao ziligonga mwamba kwani Mary hakushika simu licha ya Gidi kumpigia mara tatu.

Kufuatia hayo, Gidi alimpatia Musyoka fursa ya kumuomba msamaha mkewe hewani na kumsihi arudi nyumbani.

"Zile vitu zote nimekuwa nikikufanyia; kukuchapa, matusi na hata kukufuata fuata sitafanya tena. Nakupenda kama mke wangu na naomba urudi tuendelee na maisha. Wewe ndiye mwanamke pekee ninayempenda maishani mwangu. Sitawahi kukufanyia kitu kibaya. Nakupenda sana sana," alisema.

Je, una ushauri upi kwa Musyoka?