Patanisho:"Anakaa tu nyumbani anacheza pool, anaacha watoto na njaa" Mwanadada amlalamikia mumewe

Mokaya alisema mkewe alimdanganya kuwa anapeleka watoto wao wawili hospitalini ila hakuwahi kurudi.

Muhtasari

•"Bibi yangu akatoka kwa nyumba akasema anapeleka watoto hospitali. Aliniambia ni homa tu. Nikamwambia basi awapeleke tu, kumbe ilikuwa mpango wa kutoroka," Mokaya alisimulia.

•Mokaya aliukataa kabisa ushauri wa mke wake na kubainisha kuwa hangetaka kuondoka nyumbani kwao.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Steve Mokaya kutoka Nyamira alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Faith ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Mokaya alisema mkewe alimdanganya kuwa anapeleka watoto wao wawili hospitalini ila hakuwahi kurudi.

"Ilikuwa juzi juzi tu, bibi yangu akatoka kwa nyumba akasema anapeleka watoto hospitali. Ni watoto wawili. Aliniambia ni homa tu. Nikamwambia basi awapeleke tu, kumbe ilikuwa mpango wa kutoroka," Mokaya alisimulia.

Mokaya alisema baada ya mkewe kutoroka alizima simu yake na hivyo akachukua hatua ya kumfuatilia kupitia ndugu zake.

"Nilipigia dada yake mkubwa simu nikamuuliza kama amefika nyumbani akasema hajathibitisha. Baadaye nilimpigia mamake akaniambia msichana ako kwa nyumba. Alikataa kumpatia simu," alisema.

Mokaya alikana kuwahi kumkosea mkewe kwa namna yoyote.

Gidi alimpigia simu mamake Faith katika juhudi za kuwapatisha. Mamake Faith hata hivyo alisikika kupinga hatua ya bintiye kurudiana na Mokaya huku akidai kwamba alimtesa sana wakati wa ndoa yao.

"Mimi siwezi kuzungumza kitu juu mimi nimeokoka. Sitaki mtoto wangu asumbuliwe. Acha nikae na yeye. Alikuwa anamsumbua sana.

Ata bodaboda ambayo walitegemea alitoa vitu mpya akaweka ya zamani na ilikuwa ya mkopo. Sasa huyo ni mtu, si ni mwizi. Sasa inakaa tu kwa nyumba. Hata ameuza ploti, yenye imebaki kidogo amekodisha. Watoto wakunywe uji asubuhi, wakunywe uji mchana. Ni maisha gani hayo," alisema.

Baada ya kusema hayo, Mama Faith alimkabidhi simu bintiye ili wajaribu kuelewana na mume wake Mokaya. Faith alifichua kwamba alijaribu kumshawishi mumewe wakatafute kibarua ila akakataa kuondoka nyumbani.

"Nilimwambia tutoke nyumbani tuende tutafute kazi kwa sababu huko nyumbani ni njaa, akakataa. Yeye anakaa tu nyumbani anacheza pool.  Mimi nampenda lakini njjaa ndio ilikuwa shida. Alikuwa anaacha watoto njaa. Nilitoka angalau nikuje nifanye kibarua. Nilimwambia akuje huku tutafute nyumba tuishi tutafute kibarua akakataa," alisema.

Mokaya hata hivyo aliukataa kabisa ushauri wa mke wake na kubainisha kuwa hangetaka kuondoka nyumbani kwao.

"Mimi siwezi kuja huko. Mambo ya kutegemea mamako uachane nayo kabisa. Kwani ulikuwa unalala njaa?" Mokaya alimwambia Faith.

Faith alilalamika kwamba nyumbani kwa kina Mokaya kuna fitina sana na hangetaka kurudi huko.

Wawili hao walikubali kuzungumza baadaye ili kutafuta suluhu kuhusu mzozo wao.