Patanisho: Mwanadada amtema mumewe juu ya elimu ndogo "Sikaangi na mtu hajasoma!"

Anastacia alidai mumewe alimpasha matusi makali yaliyopelekea yeye kufanya uamuzi wa kukatiza uhusiano naye.

Muhtasari

•Mutunga alieleza kuwa walitofautiana baada ya kutupiana maneno makali kwenye simu wakati Anastasia bado akiwa kwao.

•Ghost hadi alijaribu kumuongelesha Anastacia kwa Kikamba katika juhudi za kumshawishi amsamehe mumewe lakini wapi! alikataa kata kata.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Kwenye kitengo cha Patanisho, Job Mutunga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Anastacia ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Mutunga alieleza kuwa walitofautiana baada ya kutupiana maneno makali kwenye simu wakati Anastasia bado akiwa kwao.

"Alienda kwao tarehe 28 Aprili. Nikamwambia arudi nyumbani akaniambia tupatane nimpatie nauli na nikampatia. Keshoye akaamka, kulikuwa na mazishi karibu na kwao akaenda akakaa kwao. Mpaka leo hajarudi," alisema.

Aliongeza,"Juzi alinipigia simu nikakosa kuchukua. Wakati nilichukua simu nikampigia akaniambia hakaangi na mtu hajasoma. Mimi nikamtusi. Nilisomea welding polytechic. Yeye alifika kidato cha nne."

Mutunga alisema angependa kumuomba Anastacia msamaha kwa sababu anajuta na kuhisi alimkosea sana.

"Nadai kumuomba msamaha juu nafikiri nilimkosea. Mimi niko na stress mingi sana," alisema.

Anastacia alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba hataki kuzungumza na mzazi huyo mwenzake.

"Mwambie akae maisha yake aachane na yeye. Mimi siwezi nikamuongelesha kwa sasa. Haiwezekani. Mimi siwezi kuongea na yeye," alisema.

Alifichua kwamba Mutunga alimlimbikizia matusi makali ambayo yalipelekea yeye kufanya uamuzi wa kukatiza uhusiano naye.

"Alinitusi sana. Ni mazoea. Hiyo alinitusi ilikuwa sana nikaamua yeye aishi maisha yake na mimi niishi yangu. Hadi nikimsamehe atarudia tena. Kwani hiyo siku alikuwaje ndio anitusi. Si akae maisha yake," alisema.

Mutunga ambaye alisikika kuvunjika moyo aliendelea kujaribu kumuomba radhi mkewe hewani katika juhudi za kufufua mahusiano yao.

"Mimi nilikosa lakini nilikuwa nataka kuomba msamaha. Anastacia nisamehe. Sikuwa nataka nikikosa. Mimi nateseka sana katika maisha yangu. Naomba msamaha juu naona ulinikosea kunitusi. Nilikuwa naomba unisamehe na mimi nikusamehe" Mutunga alisema kabla ya simu yake kukatika.

Anastacia hata hivyo alishikilia msimamo wake kwamba hawezi kumsamehe mumewe. Mtangazaji Ghost Mulee hadi alijaribu kumuongelesha Anastacia Kikamba katika juhudi za kumshawishi amsamehe mumewe lakini wapi! alikataa kata kata.