Patanisho: Mwanaboda aachwa baada ya mkewe kumshuku kuwa na mahusiano na mteja

Otunga alisema mkewe alimshutumu kuwa na mpango wa kando baada ya kupokea simu aliyopigiwa na msichana.

Muhtasari

•Otunga alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwezi Desemba baada ya uaminifu wake kwake kupungua.

•Otunga alijitetea kuwa msichana aliyekuwa amepiga simu yake ni alikuwa mteja wake tu bali sio mpango wa kando.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Joshua Otunga ,23, kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Brenda Olanga ,21, ambaye alikosana naye mwishoni mwa mwaka jana.

Otunga alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwezi Desemba baada ya uaminifu wake kwake kupungua. Alisema Brenda alimshutumu kwa kuwa na mpango wa kando baada ya kupokea simu aliyopigiwa na msichana.

"Desemba mwaka jana nilitoka nikaenda kazi Nairobi, nilikuwa nimeacha kazi ya boda. Nilipofika ukorofi ikatokea nyumbani. Wakati moja msichana alipiga simu nikiwa mbali akashika alafu akaongea naye wakazozana. Kwa kuwa nilikuwa bafu, nilipotoka akaniuliza kwani wako wangapi. Mimi sikuelewa," alisema.

Aliongeza, "Uaminifu ulirudi chini hadi akatoka akaenda kwao alafu baadaye akaenda Nairobi. Niliacha kazi pia nikaenda Nairobi."

Otunga alijitetea kuwa msichana aliyekuwa amepiga simu yake ni alikuwa mteja wake tu bali sio mpango wa kando.

Juhudi za kumpatanisha Otunga na mkewe hata hivyo hazikufua dafu kwa kuwa Brenda hakupokea simu licha ya Gidi kumpigia mara kadhaa.

Otunga alipopewa fursa ya kuomba msamaha hewani alisema, "Brenda naomba uweze kunipigia simu. Nilikuwa nataka kuomba msamaha kwa vile nilivyokukosea. Naumia katika maisha yangu ya sasa sio kama tulipokuwa pamoja."