Patanisho:Upweke wakumba mzee baada ya pombe, vurugu, vita, matusi kuvunja ndoa ya miaka 29

"Tulikuwa na shida fulani hatukujaliwa mtoto. Hata hivyo nimekubali kuishi na yeye kwa sababu Mungu ndiye hupeana watoto," Otengo alisema.

Muhtasari

•Otengo alisema ndoa yake ya miaka 29 ilivunjika mnamo wezi Machi mwaka jana baada ya yeye kumshambulia mkewe kwa maneno makali.

•Otengo alibainisha kwamba tayari amelipa mahari na walifunga pingu za maisha na Florence mwaka wa 2019 ila hawajafanikiwa kupata mtoto.

•Bi Florence alifichua kwamba ulevi wa mumewe na mazoea ya kumpiga zilimfanya agure ndoa yake ya miongo mitatu.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Karoli Otengo ,53, kutoka Busia alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Florence Akumu ,47, ambaye alikosana naye mwaka jana.

Otengo alisema ndoa yake ya miaka 29 ilivunjika mnamo wezi Machi mwaka jana baada ya yeye kumshambulia mkewe kwa maneno makali.

"Kwa kweli nilikuwa nimeonja kitu ya wazee kidogo. Nikakosana naye kidogo lakini sikumpiga. Huenda alichukua maneno yangu vibaya," Otengo alisimulia.

Otengo alibainisha kwamba tayari amelipa mahari na walifunga pingu za maisha na Florence mwaka wa 2019 ila hawajafanikiwa kupata mtoto.

"Hatukujaliwa na mtoto. Alinikuta na mtoto kwa ndoa nyingine. Tulikuwa na shida fulani hatukujaliwa mtoto. Hata hivyo nimekubali kuishi na yeye kwa sababu Mungu ndiye hupeana watoto," Otengo alisema.

Alisema amepiga hatua ya kuenda kwa kina Florence mara tano kwa lengo la kutafuta suluhu mzozo wao ila bado hajakubali kurudi.

"Alinielezea atanisamehea akarudi. Hadi wa leo hajarudi. Nimeshaenda kwao mara tano na akasema amenisamehea. Lakini hajarudi," alisema.

Bi Florence alipopigiwa simu, Otengo alichukua nafasi hiyo kumwomba msamaha na kumsihi arudi katika ndoa yake.

"Tafadhali nisamehe kwa makosa nilifanya. Rudisha roho chini turudiane tukae pamoja. Rudi nyumbani tuendelee kuishi pamoja kama awali," Otengo alimwambia mkewe.

Bi Florence alifichua kwamba ulevi wa mumewe na mazoea ya kumpiga zilimfanya agure ndoa yake ya miongo mitatu.

"Sioni kama nitaongea mengi kulingana na aliyonifanyia. Hii ulevi yake ya kila mara , hata sio mara ya kwanza kutoka huko. Mtu ata anakutushia maisha, kweli unaweza kukaa naye?? Alikuwa hata ananichapa," Florence alisema.

Aliendelea, "Sio mara yangu ya kwanza kutoka hapo ama kukosana. Tumekosana mara nyingi. Hiyo miaka sikufaa kutoka huko lakini vile alikuwa ananipeleka niliona hapana. Nimesema ni bora aishi maisha yake."

Otengo alijitetea, "Kitambo tulikuwa tunapigana lakini vile tumekuwa wakubwa ata nilimweleza nimeacha."

Otengo aliweka wazi kwamba iwapo mkewe atarudi atabadilisha mienendo yake na hata akaapishwa na Ghost.

Florence hata hivyo alibainisha kwamba bado anahitaji muda wa kufikiria kabla ya kufanya maamuzi kuhusu kurudi.

"Enyewe si vizuri. Ata mimi sikufurahia. Najua ameapa lakini tabia ni ile ile. Akae kwanza maisha yake. Nikifikiria nitarudi," alisema.

Maneno yake ya mwisho, Otengo alimwambia mkewe, "Mke wangu Florence huwa nakupenda sana. Jinsi tuliapa kanisani tukasema tutavumilia, rudi nyumbani na usiwe na uoga na urudi nyumbani uendelee na kazi yako kama mke wa boma. Nakupenda kama samaki ya tilapia ikiwa imepikwa."

Florence alimwambia avumilie tu.