Patanisho: Jamaa atishia kujinyonga, kupatia watoto sumu baada ya kuachwa na mkewe

"Walinivamia na mamake wakanigonga mpaka nikaenda hospitali Kenyatta nikafanyiwa upasuaji," Mercy alilalamika.

Muhtasari

•Samuel alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 13 ghafla baada ya kutofautiana kuhusu kutazama mchuano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

•Mercy alifichua kwamba Samuel alikataa kulipa mahari licha ya kuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

.Samuel Ingutsia ,36, kutoka Kakamega alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mercy Mukolwe ,29, ambaye alikosana naye wiki jana.

Samuel alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 13 ghafla baada ya kutofautiana alipotaka kuenda kutazama mchuano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

"Mimi nafanya kazi ya bodaboda. Siku moja nilitoka kazi  usiku nikaambia mke wangu naenda kuona mpira. Ilikuwa mechi baina ya Real Madrid na Man City. Hakutaka niende kuona mpira na hapo tukaaza kuzozana," alisema.

Aliongeza, "Hiyo ndo ilifanya tukosane akaenda. Nilitoka asubuhi iliyofuata nikaenda kazi, kurudi nilipata ameenda.. Saa hii tunazungumza kwa simu tu lakini kurudi ni shida. Sikunywi pombe. Mimi ni wa kanisa. Mipango wa kando sina, ni pikipiki tu nikitafuta kazi."

Mercy alipopigiwa simu alifichua mengi kuhusu mume wake. Alidai kwamba mumewe ni mvivu, mwenye vurugu na hana heshima kwa wazazi wake.

Aidha, alisema Samuel alimshuku kila mara alipoona wateja wanaume katika eneo lake la biashara.

"Mtu kama anaweza kudharau wazazi wangu nitakaa na yeye aje sasa. Hataki kufanya kazi. Mara pikipiki inamsumbua. Mkikosana kidogo anakupiga. Ni mazoea. Wazazi wake kila siku ni kelele 

Mimi ni mwanabiashara. Nikifanya biashara akipata wanaume anasema wananitongoza," Mercy alisema.

Samuel hata hivyo alisema, "Huyo mke wangu sijawahi kumpiga. Wazazi wangu ndo wanampiga vita sio mimi."

Alisema mumewe na mama mkwewe walikuwa na mazoea ya kumshtumu kwa kukosa kupata mtoto mwingine baada ya upasuaji.

"Walinivamia na mama yake wakanigonga mpaka nikaenda hospitali Kenyatta nikafanyiwa upasuaji na kulazwa.  Nilifanyiwa upasuaji huko kwao. Kila mara alinitusi eti siwezi kuzaa. Alikuwa ananitusi pamoja na wazazi wake," alisema.

Mercy alifichua alijaribu kumshauri mumewe apige hatua ya kuenda nyumbani kwao ili kujaribu kusuluhisha mzozo wao ila akapuuza.

"Uliniambia nikitoka huko niende na niende ati hutawahi kunitafuta. Wewe oa bibi mwingine. Nitakujia watoto wangu lakini huko kwenu nimetosheka. Nilikwambia ukuje kwa mama tusuluhishe maneno ukakataa. Sasa umechelewa, mimi nishatoka huko niko Nairobi," Mercy  alisema.

Aidha, alifichua kwamba Samuel alikataa kulipa mahari licha ya kuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja.

"Alisema kama nitaona ng'ombe wakienda kwetu nitakuwa naota.. Sasa anakaa akitume jumbe vile anataka kujinyonga na apatie watoto sumu. Anatumia mpaka mama yangu, haogopi mama mkwe," alisema.

Aliweka wazi kwamba hana mpango wa kurudi kwa ndoa yake ila akasema ataenda kuwachukua watoto wao.

"Mimi sirudi huko, naendea watoto wangu. Nilijaribu sana akuje nyumbani akakataa. Mwambie atafute mwingine," alisema.

Samuel alimwambia Mercy, "Naomba kama unapenda urudi, sina mpango wa kuoa mwingine."

Je, una ushauri upi kwa wawili hao?