Patanisho: Mwanadada akatalia kwao baada ya mumewe kulipa mahari

"Unatakaje nirudi na umeoa tayari. Siwezi nikarudi. Uko na mchezo," Gacheri alimwambia Saitoti.

Muhtasari

•Saitoti alisema alienda Meru kumlipia mahari mkewe ila baada ya mikakati yote kukamilika Gacheri akakosa kurudi naye nyumbani.

•Saitoti alibainisha kuwa Gacheri ndiye mke wa kwanza, jambo ambalo mke wake wa pili anafahamu vizuri.

Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, mwanaume aliyejitambulisha kama Jackson Saitoti (38) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Caroline Gacheri (25 ambaye alitengana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Saitoti alisema alienda Meru kwa ajili ya kumlipia mahari mkewe ila baada ya mikakati yote kukamilika Gacheri akakosa kurudi naye nyumbani.

"Tulikaa na mke wangu kwa ndoa kwa miaka mitano na tulikuwa na watoto wawili.Tukikosana kwa mambo ya simu lakini tukasuluhishaIkafika wakati wa kupeleka mahari. Tukafika huko kwao tukalipa mahari. Sikuwa nimeenda kwao. Alisema atakaa kwao ili wazazi wake wamfunze jinsi ya kukaa na mwanaume," Saitoti alisema.

"Tulienda nyumbani nikangoja mwanamke lakini hakuja.Niko na mwanamke mwingine lakini sio shida kwa sababu baba yangu ana wanawake wawili na baba yake ako na wanawake wawili. Tulienda na wazazi wangu tukalipa mahari. Baadaye akawa hakuji mpaka leo hajakuja. Ilikuwa 2021," alisema.

Bi Gacheri alipopigiwa simu alisikika kushangaa kwa nini mzazi huyo mwenzake alikuwa anamtafuta ilhali tayari ameoa.

Aidha alieleza kwamba Saitoti alitoa kiasi fulani cha pesa kwa wazazi wake ila hazikuwa mahari.

"Hiyo miaka yote. Huyo jamaa hayuko serious., Alitoa mahari gani?? Alitoa kitu lakini sio mahari. Hakutoa yote. Huyo jamaa anasumbua," Gacheri alisema.

"Unatakaje nirudi na umeoa tayari. Siwezi nikarudi. Uko na mchezo," alimwambia Saitoti.Saitoti alisisitiza kwamba kuwa na mke mwingine sio hoja kwani baba yake pia alikuwa na wake wawili.

Aidha alibainisha kuwa Gacheri ndiye mke wa kwanza, jambo ambalo mke wake wa pili anafahamu vizuri.

"Baada ya yeye kuenda nikachukua mwingine. Mtu hawezi kukaa bila mwanamke. Hata huwa nampigia simu Gacheri nikiwa na mke huyo mwingine na hana shida," Saitoti alisema.

Gacheri alidokeza kwamba ndoa yake na Saitoti ilikuwa sumu, jambo ambalo lilichangia yeye kukataa kurudi."Alifanya harusi ya kimaasai.

Alikuwa ananitumia picha zake za harusi. Yule mtoto wa kwanza hata kabla ya kumaliza mwaka, alikuwa amenipa mtoto mwingine, hata hakungoja nipone, halafu hatambui mtoto msichana, ana ubaguzi wa watoto kisa na maana, mtoto msichana sio wake," Gacheri alisema.

Aliendelea, "Hajatoa mahari, alitoa tu kidogo amezoea kunitishia. Mwambie akate simu atulie,. Yeye ni baba kwa jina tu, analea watoto kwingine lakini wake hawatunzi."

Saitoti alisisiza kwamba anamtaka mzazi huyo mwenzake arudi ili waweze kulea watoto wao wawili pamoja.

Gacheri hata hivyo alimwagiza aweze kuwashughulikia watoto kwanza kabla ya hatua nyingine yoyote.