Patanisho: "Akili haiko sawa, imekorogeka" Jamaa asononeka wiki moja baada ya kuachwa na mpenziwe

"Kutoka jana akili yangu haiko kabisa. Akili yangu imekorogeka. Nimeshindwa hadi kuelewa. Nimechanganyikiwa kabisa," Peter alilalamika.

Muhtasari

•Peter alieleza kuwa ndoa yake ya mwaka mmoja unusu ilisambaratika baada ya mkewe kumshuku kuwa na mipango wa kando. 

•Gidi pia aliwashauri vijana dhidi ya kuwapenda wasichana wa takriban miaka 21 kwa roho yote.

Image: RADIO JAMBO

Peter Shabaya ,32, kutoka Changamwe alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Eunice Awori ,21, ambaye alikosana naye takriban wiki moja iliyopita.

Peter alieleza kuwa ndoa yake ya mwaka mmoja unusu ilisambaratika baada ya mkewe kumshuku kuwa na mipango wa kando. 

"Nikienda kwa nyumba nikiwa nimechelewa anauliza natoka wapi usiku. Namwambia ni sababu ya kazi. Alikuwa ananishuku niko na wasichana ila si kweli. Sikuwa na mpango wa kando. Sikuwa na msichana yeyote," Peter alisema.

Aliongeza, "Alikuwa ananishuku kwa sababu ya kuingia kwa nyumba usiku. Huwa nampigia simu lakini hatuelewani. Hata jana nilimpigia lakini hatukuelewana. Nasononeka sana hata mawazo ni mengi. Najiuliza mbona iko hivi."

Peter alisema mkewe alihamia kwa kaka yake baada ya kuondoka.

Kwa bahati mbaya, Eunice hakupatikana kwa simu wakati alipopigiwa na Gidi.

Peter alisema, "Hata jana tulikorofishana akaniambia anaweza kuzima simu. Kutoka jana akili yangu haiko kabisa. Akili yangu imekorogeka. Nimeshindwa hadi kuelewa. Nimechanganyikiwa kabisa. Niko kazini lakini ni kujaribu tu "

Peter alibainisha kwamba anampenda mama huyo wa mtoto wake mmoja kwa roho yake yote

Alipopewa fursa ya kuzungumza naye hewani alisema, "Eunice nakuomba rejesha roho yako chini tuongee. Sijawahi kukusea maishani, hii ni mara ya kwanza. Nakupenda na roho yangu yote. Nakuomba msamaha."

Huku akimshauri kuhusu jinsi ya kukabiliana na anayopitia, Gidi alimwambia Peter, "Usimpigie simu sasa hivi mpaka atakapotulia. Akitulia mtazungumza. Huenda bado amekasirika ndio maana mnakorofishana. Mpe muda atulie."

Gidi pia aliwashauri vijana dhidi ya kuwapenda wasichana wa takriban miaka 21 kwa roho yote.

Je, ushauri wako kwa Peter ni upi?