Patanisho: Jamaa aachwa na mpenziwe kwa kumpost Facebook

"Nilipost picha yake FB lakini hakuataka hivyo. Yeye alitaka nimuulize kwanza," Kiplimo alisema.

Muhtasari

•Kiplimo alisema kwamba mahusiano yake ya miaka miwili yalifika kikomo baada ya mpenziwe kughadhabishwa na hatua yake kumpost kwenye Facebook bila idhini yake.

•Kiplimo aliweka wazi kwamba bado hajapata mwanadada mwingine wa kuridhisha moyo wake kwani anamkubali sana Sharon.

Image: RADIO JAMBO

Nehemiah Kiplimo ,25, kutoka Nandi Hills alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Sharon Chepkosgey ,22, ambaye alikosana naye takriban miaka mitatu iliyopita baada ya kutofautiana kidogo.

Kiplimo alisema kwamba mahusiano yao ya miaka miwili yalifika kikomo baada ya mpenziwe kughadhabishwa na hatua yake kumpost kwenye mtandao wa Facebook bila idhini yake.

"Nilipost picha yake FB lakini hakuataka hivyo. Yeye alitaka nimuulize kwanza," Kiplimo alisimulia.

Aliendelea, "Nilikuwa nimeamua atakuwa mke wangu. Alikasirika akaja kuniuliza kwa nini nilimpost. Nilimwambia mimi nilikuwa nampenda na nikaamuliza kwa nini alitaka nimuulize kwanza kabla ya kupost. Tulikosana akaniambia niende nifikirie kwanza naye pia afikirie."

Kiplimo alibainisha kwamba licha ya kukosana, bado huwa anawasiliana na Sharon kwa njia ya simu ila amekuwa akimsihi ampe muda.

"Mara ya mwisho tuliongea ni mwezi wa tano mwaka huu. Tuliongea lakini alikuwa anataka credit ndio anipigie. Yeye alitaka anipigie lakini mimi nikimpigie hataki. Nataka nijue yeye ameamua aje. Mimi siko sawa kabisa," alisema.

Aliweka wazi kwamba bado hajapata mwanadada mwingine wa kuridhisha moyo wake kwani anamkubali sana Sharon.

Sharon alipopigiwa simu Kiplimo alichukua fursa hiyo kukiri makosa yake na kuomba msamaha.

"Sharon nilifanya makosa kukupost FB. Acha turudiane tuendelee na maisha yetu," Kiplimo alimwambia Sharon.

Sharon alisema, "Tutaongea na yeye.. Yeye hakuniambia akipost. Kuna matumaini tunaweza kurudiana . Bado sijapata mwanaume mwingine.

Kiplimo alisema anasubiri sana aweze kurudiana na mchumba huyo wake.

"Sharon mimi bado nakupenda. Nakujali sana. Nataka tukae na wewe Nampenda kama asali," Kiplimo alisema.

Sharon hata hivyo alikata simu kabla ya kusema maneno ya mwisho.