Patanisho: Jamaa aachwa kwa kumpiga mkewe mara 5 hadi kumvua nguo mbele ya mtoto

Githinji alisema ndoa yake ya miaka minane mwezi Februari baada ya kumshambulia mkewe akiwa mlevi.

Muhtasari

•“Nililewa na marafiki. Pombe tu ndio ilifanya nikampiga bibi haikuwa mara ya kwanza kulewa lakini nikama haikuwa sawa,” Githinji alisimulia.

•Joseline alisema kwamba tayari amemsamehe mume huyo wake wa zamani ila akaweka wazi kwamba hakuna nafasi ya kurudiana.

Image: RADIO JAMBO

Kelvin Githinji ,28, kutoka Chuka alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Joseline Kawira ,25, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.

Githinji alisema ndoa yake ya miaka minane mwezi Februari baada ya kumshambulia mkewe akiwa mlevi.

“Nililewa na marafiki. Pombe tu ndio ilifanya nikampiga bibi haikuwa mara ya kwanza kulewa lakini nikama haikuwa sawa,” Githinji alisimulia.

Aliongeza,”Mke wangu tumekuwa tukizungumza naye lakini aliniambia nimpatie muda atareJea. Nimekuwa nikilipia mtoto karo ila juzi aliniambia nimtumie transport ya mtoto ya shule lakini sikuwa nimelipwa."

Githinji aliweka wazi kuwa licha ya kuachana, wamekuwa wakizungumza na hata kuonana mara moja moja.

“Tulionana wiki jana. Nilimpigia simu akaniambia yuko busy, nikamwambia apatie mtoto simu tuongee na yeye akasema mtoto yuko busy pia. Baadaye alipiga nikakataa kushika simu pia,” alisema.

Joseline alipopigiwa simu, Githinji alitumia fursa hiyo kumuomba msamaha kwa makosa ambayo aliwahi kumtendea.

"Nimekumiss sana nimechoka na kukungoja nikaona nipige simu radio jambo nione kama nitasaidika, hata kama nilikukosea nisamehe sitaki kuoa bibi mwingine na wewe uko,” Githinji alimwambia mzazi huyo mwenzake.

Joseline alisema kwamba tayari amemsamehe mume huyo wake wa zamani ila akaweka wazi kwamba hakuna nafasi ya kurudiana.

Alifichua kwamba mzazi huyo mwenzake ni mtu wa vurugu na aliwahi kumpiga mara yasiyopungua tano.

“Sio mara ya kwanza, alinipiga mara tano mpaka akanitoa nguo mbele ya mtoto.Ilikuwa ni mazoea tumeongea mpaka na wazazi ikashindikana mimi nikaona nijiondoe kwa ndoa kabla nife. Nilimsamehe lakini hatuwezi kurudiana. Sirudi, Sirudi!!." Joseline alisema.

Mama huyo wa mtoto mmoja alifichua kwamba hapo awali wamewahi kushiriki kikao na wazazi na akakubali kurudi ila baada ya wiki mbili mumewe akampiga na kumfanya atoroke tena.

Githinji hata hivyo aliendelea kumshawishi arudi huku akimueleza kwamba hata ameacha tabia ya kunywa pombe.

"Mtu hawezi badilika mara moja tu, mimi kama sijalewa sijawahi mpiga kwahivyo niliweka pombe chini, miezi mbili sasa sijalewa,” alisema.

Joseline hata hivyo alishikilia msimamo wake na hata kumpa Githinji idhini ya kuoa mke mwingine.

“Mwambie aoane, kama anaoana aoane,” alisema.

Githinji alipopewa nafasi ya kumwambia maneno ya mwisho kwa mzazi huyo mwenzake alisema, “Nimekuja kugundua makosa ilikuwa yangu ndio maana nimeomba msamaha. Nakupenda sana ndio maana nakuhitaji maishani mwangu.”

Joseline alisema, “Sina maneno ya kumwambia.”