Patanisho: Jamaa atishia kujitoa uhai mkewe akitazama baada ya ndoa ya miaka 3 kuvunjika

Ondieki alimtaka mkewe kusubiri hadi mwaka uishe kabla ya wao kurudiana.

Muhtasari

•Mueni alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwezi Mei baada ya mimba aliyokuwa amebeba kuharibika.

•Ondieki hata hivyo alishikilia msimamo wake kuwa mkewe asubiri hadi mwaka uishe kabla  ya kufanya maamuzi.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Anastacia Mueni ,29, kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Dennis Ondieki ,35 ambaye alitengana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Mueni alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilisambaratika mwezi Mei baada ya mimba aliyokuwa amebeba kuharibika.

"Mume wangu alinioa na watoto wawili. Huyo mdogo alikuwa mdogo kabisa, yeye ndiye amemlea. Nilipata mimba alafu mwezi wa nne ikatoka. Hapo awali alikuwa anakuja kwa nyumba kama amekasirika. Nikimuuliza hataki kuniongelesha, nikapata pressure hadi mimba ikatoka," Mueni alisimulia.

Mueni alifichua kuwa shida zaidi zilikumba ndoa yao baada ya kupoteza ujauzito kwani mumewe hakumtaka nyumbani.

"Alikuwa ananifukuza akiniambia ati nitoke anataka kukaa pekee yake. Nilitoka nikakodisha nyumba nikaanza kuishi pekee yangu. Baadaye alinipigia simu nikamwambia mimi nimekodisha nyumba kwingine kwani hanitaki. Akauliza kwani nimepata mwanaume mwingine," Mueni alisema.

Mueni alisema kufuatia hayo mumewe alianza kutishia kujitoa uhai.

"Alisema amekuwa akinitafuta ajiue akiona, nikamwambia ajiue nikiona. Yeye hakutaka kunionyesha mahali anaishi. Nilikuwa nikimuuliza anataka aje lakini hakutaka kuniambia. Amekuwa akinipigia simu na kuaniambia asiwahi kuniona na mwanamke mwingine. Nataka kujua msimamo wake," alisema.

Bw Ondieki alipopigiwa simu alibainisha kwamba yuko kazini na kudai kuwa angempigia Mueni simu baadaye.

Mueni hata hivyo alichukua fursa hiyo kumhakikishia mpenzi huyo wake kwamba yuko tayari kwa hatua ambayo angetaka wachukue.

"Nimekaa nikishangaa kwa nini hujaniambia umeendelea na maisha yako ili pia mimi niendelee na maisha yangu. Ukiniambia umeendelea na maisha yako niendelee na yanguawa. Ukitaka turudiane mimi niko tayari," Mueni alimwambia mumewe.

Ondieki alisema, "Nitakupigia simu baadae.Nilikuwa nampenda lakini nilienda kwao akaniongelesha vibaya. Nilimwambia atulie kwanza mpaka mwaka huu uishe."

Mueni hata hivyo alisema," Mimi naona hiyo sio sawa. Mtu ambaye tumekaa naye zaidi ya hiyo miaka mitatu anasema anataka kukaa peke yake saa hii, nini kibaya ameona kwangu sasa."

Ondieki hata hivyo alishikilia msimamo wake kuwa mkewe asubiri hadi mwaka uishe kabla  ya kufanya maamuzi.

"Sawa basi, wacha nikubaliane na yeye. Ukiona mimi nimepiga simu, mimi nimebadilika. Nyumbani alisema ananipenda lakini tutaishi kando, nikasema sio sawa. Kama amesema hivyo wacha ningoje," Mueni alisema.

Ondieki alisema alichukua uamuzi huo ili mkewe ,"Ndio ajue mwanaume hafai kufanyiwa kitu kama hiyo."

Mueni aliendelea kulalamika, "Kutoka mbali nilikupenda kama mume wangu. Nitakaa muda wote nikiwaza . Umenipea muda mwaka mzima nitaishi na nani?"

UJe, ushauri wako kwa wawili hao ni upi?