Kijana wa miaka 25 asononeka baada ya kuachwa na mkewe wa miaka 31 kwa kubagua wanawe

Leonida alidai mumewe alikuwa akimnunulia mtoto wake chakula kizuri na kuwaacha wake wawili wale sukuma bila nyanya.

Muhtasari

•Achoki alisema ilivunjika mwezi Mei 2021 wakati mkewe alipoondoka baada ya kumshtumu kwa kubagua watoto wake wawili na kupendelea wake mmoja.

•Leonida aliweka wazi kwamba alihamia Lamu pamoja na watoto katika harakati za kuwatafutia chakula.

Image: RADIO JAMBO

Bw Geoffrey Achoki Omweri ,25, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Leonida Semu ,32, ambaye alikosana naye takriban miaka miwili iliyopita kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Achoki alisema ndoa yake ya miaka minne ilivunjika mwezi Mei 2021 wakati mkewe alipoondoka baada ya kumshtumu kwa kubagua watoto wake wawili na kupendelea wake mmoja.

"Tumekaa na yeye  miaka miwili tukakosana mwaka wa 2021. Alisema nabagua watoto wake na napenda yule wangu. Nilimwambia sina ubaya na watoto. Akasisitiza ameona niko na ubaguzi. Nikamwambia nataka kuenda nyumbani niko na shughuli. Kurudi Nairobi nikapata nyumba iko pekee yake amebeba kila kitu," Achoki alisimulia.

Aliongeza, "Nilipiga simu kwao nikaulizwa nalalamika kwa nini na hakuna kitu nimepeleka hata paka. Nikaambiwa nimtafute mwenyewe.Mimi sikuwa nawabagua watoto wake, ni vile nikitoka nilikuwa naletea mtoto wangu surprise juu ni mdogo. Watoto wake, mmoja alikuwa na miaka mitatu na mwingine minne. Huyo mmoja tumezaa na yeye. Alienda na wote. Huwa tunaongea kwa simu anasema atarudi nimpatie muda. Sijawahi kushughulikia watoto. Natumanga tu mara moja mwezi tu ukiisha. Kusema kweli, wakati alikuwa kwao nilikuwa namsaidia. Vile alienda Mombasa sijawahi kumsaidia kwa sababu sijui anafanya nini huko."

Leonida alipopigiwa simu alisisitiza kwamba Achoki alikuwa anabagua watoto wake na hata kuwapiga vibaya.

Alidai kwamba mzazi huyo mwenzake alikuwa akimnunulia mtoto wake chakula kizuri na kuwaacha wake wawili wale sukuma bila nyanya.

"Alinipata na watoto wawili, nikapata mmoja naye. Ikawa hata chakula analeta anabagua watoto wangu analetea wake tu. Kichapo kikawa ni kama mbwa. Mateso kwa nyumba na chakula haleti. Mtoto wake akila nyama wangu walikuwa wanakula sukuma bila nyanya na anapika mwenyewe. Aliwadharau. Nashukuru Mungu ni wazima nawalea," Leonida alisema.

Achoki  alisistiza kwamba amerekebika na kumuomba mkewe akubali warudiane na waendelee kuishi pamoja.

Leonida alimwambia, "Kama utaacha ubaguzi sijakataa kurudi. Kwanza nitumie pesa za mtoto leo nione kama umebadilika. Sikatai kurudi, nilienda kutafutia watoto.  Ambia kina Gidi uamuzi wako nitaskia nijue kama nitarudi."

Leonida aliweka wazi kwamba alihamia Lamu pamoja na watoto katika harakati za kuwatafutia chakula.

Alifichua kwamba Achoki ni muongo na huenda asitimize ahadi zake.

"Yeye ni muongo, atadanganya atanitumia leo na hatatuma. Tuliachana mtoto akiwa na mwaka moja, saa hii ako na miaka minne, hajui anakula nini," alisema.

Kuhusu pengo kubwa kati ya umri wao, alisema, "Ni ukweli nimemuacha na miaka saba. Niliamua kuwa na yeye juu yeye ndiye alinitaka . Nilimuuliza haoni ni mdogo. Nikamuuliza kama atatimiza matakwa ya watoto wangu na kushughulikia kila kitu changu. Nilimpenda hakuwa na kazi nikang'ang'ana na vibarua."

Achoki alimwambia, "Mimi kuanzia leo nimebadilika. Nakuomba urudi nyumbani tuendelee na maisha yetu, nakupenda sana, nampenda."

Leonida kwa upande wake alisema, "Nampenda lakini ashughulikie watoto. Nampenda yeye ni mume wangu."