"Siwezi kosa mtu, mimi ni mdogo sana!" Mwanadada atishia kurudi soko mumewe asiposema msimamo

Siwezi kosa mtu, ata ningetaka kuenda ningekuwa nishaenda. Yeye anawaogopa baba na mama mkwe," Dorothy alisema.

Muhtasari

•Dorothy alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika baada ya uhusiano wake na baba mkwe kudhoofika.

•Dorothy aliweka wazi kwamba angetaka kujua msimamo wa Orani na kutishia kusonga mbele na maisha yake iwapo hamtaki.

Image: RADIO JAMBO
 

Katika kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Dorothy Nyanchoka ,22, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Orani Nyambati ,31, ambaye alitengana naye kufuatia mzozo wa nyumbani.

Dorothy alisema ndoa yake ya chini ya mwaka mmoja ilisambaratika baada ya uhusiano wake na baba mkwe kudhoofika.

"Tulikuwa tunakaa na mume wangu. Ilifika mahali baba yake akasema nimeenda kucheza densi kwa nguru, kwa nguru ni mahali sukari nguru huwa inasiagwa. Hakukuwa na muziki, nilishangaa nacheza aje bila ngoma," Dorothy alisimulia.

Aliendelea, "Ilifika siku ingine tukaenda kwa shamba na wifi akasema ati mama yake alisema nilimfinya shingo. Nikaenda nikauliza mama kuhusu hayo, sijui waliambia baba mkwe nini  akaamka kunipiga. Saa hii niko nyumbani kwetu."

Dorothy alisema licha ya kutoroka ndoa yake amekuwa akizungumza na mumewe ambaye bado hajakuwa wazi kuhusu msimamo wake.

"Nikimpigia simu inafika mahali anasema kama sirudi ataoa. Wazazi wake walisema niende na mtu aeleze kwa nini nilikuwa nacheza. Kutoka kwetu hadi kwao ni miaka nane kwa hivyo watu wawili ni 1600 ambazo ni nyingi," alisema.

Dorothy aliweka wazi kwamba angetaka kujua msimamo wa Orani na kutishia kusonga mbele na maisha yake iwapo hamtaki.

"Mimi siwezi kosa mtu, I am too young. Siwezi kosa mtu, ata ningetaka kuenda ningekuwa nishaenda. Yeye anawaogopa baba na mama mkwe," alisema.

Gidi alipopiga simu ambayo Dorothy alitoa, jamaa aliyejitambulisha kama Dougi alichukua simu na kubainisha kuwa yeye sio Orani aliyekuwa akitafutwa na mwanadada huyo.

Dorothy hata hivyo alidai kuwa mumewe ndiye aliyeshika simu wa kwanza kisha akapatia mtu mwingine asiyejua kuzungumza.

Baadaye alidokeza kwamba alikosea namba kabla ya simu yake kukatika.

Je, ushauri wako kwa Dorothy ni upi?