"Mapenzi siku hizi hakuna!" Mwanadada amruka mkewe ambaye ameishi naye miaka 7

Mwanzoni Emily alisikika kumkana Samson kuwa mumewe na kupinga walikuwa wanaishi pamoja.

Muhtasari

•Samson alisema mkewe alihama baada ya wao kuvurugana kufuatia yeye kupoteza kazi na kushindwa kutekeleza  majukumu nyumbani.

•Samson aliweka wazi kwamba ameelewa malalamishi yote ya mkewe na kubainisha kuwa atajaribu kurekebisha.

Image: RADIO JAMBO

Samson Onyango ,38,kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Emily ,34, ambaye alimuacha miezi miwili iliyopita.

Samson alisema ndoa yake ya miaka 7 ilivurugika miezi miwili iliyopita wakati mkewe alipohama na kupanga nyumba kwingine baada ya wao kuvurugana kufuatia yeye kupoteza kazi na kushindwa kutekeleza  majukumu nyumbani.

"Wakati nilikosa ajira, yeye alikuwa anafanya kazi yake. Alianza kuona kama nimeshindwa kutekeleza majukumu yangu. Shida ingine ilikuwa nilikuwa nakunywa pombe. Hakuniambia chochote, alitoka tu akaenda," Samson alisema.

Aliongeza, "Nilikuwa naomba kumuomba msamaha. Kazi bado sijapata lakini pombe nimeacha."

Emily alipopigiwa simu, Samson alichukua fursa hiyo kumuomba msamaha.

Hata hivyo, mwanzoni Emily alisikika kumkana Samson kuwa mumewe na kupinga walikuwa wanaishi pamoja

"Si bwanangu. Kwani tulikuwa tunaishi na yeye wapi mahali nilihama? Hili suala letu ni ngumu sana. Ata yeye anajua. Ni kitu yenye siwezi kuweka hewani. Ata yeye akae chini kama mwanaume asuluhishe," Emily alisema.

Aidha, alilalamika kuhusu mume wake kutotoa mahari yoyote kwa ajili yake, jambo ambalo ameshindwa kuvumilia.

Aliongezea, "Kuna yale anafaa kufanya kama mwanaume. Hakuna kitu amenikosea. Ni tu majukumu yake anafaa atekeleze vizuri. Siwezi nikasema shida. Hili suala letu ni ngumu sana. Mimi sasa nishakuwa mtu mkubwa. Kama anataka tuishi hivyo bila mahari itakuwa ngumu. Kuna vitu mingi anafaa atekeleze majukumu yake. Niko na kijana mkubwa, nitaishi kwa hizi nyumba za kupanga mpaka lini? Kama mahari hajalipa, mimi nabaki nashangaa kama ananichezea tu ama nini."

Samson aliweka wazi kwamba ameelewa malalamishi yote ya mkewe na kubainisha kuwa atajaribu kurekebisha.

"Nitajaribu niwezavyo nitekeleze ambayo nafaa kutekeleza," alisema.

Emily alisema, "Afanye tu vitu anafaa kufanya.. Mapenzi siku hizi hakuna."