Patanisho: Jamaa akataa katakata kumwambia mke wake "Nakupenda"

Lucy alimhakikishia baba huyo wa mtoto wake kuhusu mapenzi yake mazito kwake na kumsihi warudiane.

Muhtasari

•Lucy alisema ndoa yake ya miaka 3 ilianza kuyumba mapema mwezi huu baada ya mumewe kumigia simu usiku akakosa kushika.

•Edwin alidokeza kuwa kumekuwa na mawasiliano mabaya kati yake na mkewe na kudai kuwa atampigia simu waongee.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Lucy Kanini ,22, kutoka Makueni alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Edwin Makumba ,26, ambaye alikosana naye takriban wiki mbili zilizopita.

Lucy alisema ndoa yake ya miaka 3 ilianza kuyumba mapema mwezi huu baada ya mumewe kumigia simu usiku akakosa kushika.

"Nilienda nyumbani, akapiga simu usiku kama nimelala, sikuskia. Asubuhi nilipompigia simu hakushika, jioni nikapiga akakata. Jumamosi pia nilimpigia akakosa kushika. Jumapili nilipompigia alikata na kunipigia baadaye ambapo aliniambia mwenye nilikuwa naye aliponipigia niwe nampigia tunaongea naye. Nilijaribu kumweleza akakata simu. Sasa nikimpigia simu hashikangi anakata," Lucy alisema.

Lucy alieleza kuwa yeye kukosa kupokea simu ilimfanya mumewe ashuku kwamba alikuwa na mwanaume mwingine.

Alisema mumewe amekuwa akikataa kumtumia nauli ili aweze kurudi nyumbani.

"Nilichukua namba alikuwa amenitumia pesa nayo, ni rafiki yake. Nikamuuliza kama huwa anamuona akasema hapana lakini anaweza kuniunganisha naye. Vile aliskia nimemuulizia akasema huyo mwenye nimepigia simu  niende anioe na mtoto awe wake," alisema.

Aidha, Lucy alikiri kuwa kuna binamu yake ambaye huwa anaongea naye sana na ambaye huwa anazungumzia mengi naye.

Edwin alipopigiwa simu alibainisha kuwa yuko bize na hawezi kuzungumza mengi.

Hata hivyo, alidokeza kuwa kumekuwa na mawasiliano mabaya kati yake na mkewe na kudai kuwa atampigia simu waongee.

"Kuna mambo mengi yenye siwezi kuongea hewani. Mwanzo niko bize. Anajuatu nampenda. Kumekuwa na miscommunication kidogo lakini tutaongea.Mimi sina wasiwasi naye. Tutapangana naye," Edwin alisema.

Lucy alimhakikishia baba huyo wa mtoto wake mmoja kuhusu mapenzi yake mazito kwake na kumsihi warudiane.

"Bado mimi nakupenda kama baba ya mtoto wangu. Sitaki utuache. Tuendelee tu na maisha pamoja," alisema.

Edwin alipoombwa amwambie mke wake Lucy kuwa anampenda alionekana kusitasita na kusema tu, "Anajua nampenda."

Lucy alisema, "Ata simu yenyewe anaweza kosa kupiga. Sinauhakika."

Je, ushauri wako ni upi?