Patanisho: Jamaa aliyeachwa alalamika kutapeliwa na wanawake wanaoiga sauti ya mkewe

"Nimekuliwa pesa sana na wasichana wanabadilisha sauti wakisema ni Carol," Erick alilalamika.

Muhtasari

•Erick alikiri kuwa uhusiano wake na mama mkwe, mke wake uliharibika baada ya kusingiziwa madai ya jaribio la unajisi na kuzuiliwa katika rumande kwa mwaka mmoja na miezi minane.

•Mama Carol alipopigiwa simu alimshtumu Erick kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake na binti yake. 

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Erick Makoi Zinka kutoka Uganda alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama mkwe wake Mama Carol ambaye mawasiliano yake naye yalikatika baada ya kuzuiliwa rumande.

Erick alikiri kuwa uhusiano wake na mama mkwe, mke wake uliharibika baada ya yeye kusingiziwa madai ya jaribio la unajisi na kuzuiliwa katika rumande kwa mwaka mmoja na miezi minane.

"Nilikuja nikaoa msichana hapa Nairobi. Tukakaa tukapata mtoto msichana 2021. Nikapata kazi Kawangware tukaenda. Nikapata shida kwa ploti. Kuna mama alikuwa akitaka mahusiano na mimi. Nikakataa. Akasema atanifunza funzo na sitawahi kurudi Nairobi. Akawa analetea bibi yangu maneno. Bibi yangu akawa amekasirika," Erick alisimulia.

Aliendelea, "Wakati nilikataa mahusiano naye, alikuja akanishtaki. Alisema nimeshika watoto wake wawili. Kwa kuwa sikutaka kuzozana naye nikamwambia twende mbele. Nimekaa huko Industrial area mwaka moja miezi nane, lakini nikashinda kesi. Tulikuwa tunaongea na mama mkwe lakini wakati nilitoka mawasiliano yalikatika. Sasa imefika mahali hata hachukui simu. Nataka kujua msiamo wao.

Nilihama Kawangware nikaenda Zambezi. Sijui mahali mke wangu ako. Niliambiwa hana simu. Nilikuwa nimeshtakiwa na jaribio la unajisi. Mke wangu nampenda na sina amani kabisa. Mara ya mwisho ilikuwa mwezi wa tano 2021 kabla ya kwenda rumande."

Mama Carol alipopigiwa simu alimshtumu Erick kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake na binti yake. 

Pia alidai kwamba uhusiano kati ya wanandoa hao wawili tayari ulikuwa umeharibika hata kabla ya Erick kuzuiliwa.

"Ukipata mtu alafu unaanza kutafuta wengine huko nje unadhani atafikiria nini? Wewe ilikuwa hamuelewani vizuri. Mke wako hajarudi. Alikuwa anamuonyesha madharau. Ata hawakuwa wanaelewana kwa nyumba," alisema Mama Carol.

Erick alimuomba mama mkewe amsaidie namba ya Carol ili aweze kuwasiliana naye moja kwa moja huku akidai kwamba amekuwa akitapeliwa na wanadada wengine ambao wamekuwa wakidai ni mkewe.

"Nimekuliwa pesa sana na wasichana wanabadilisha sauti wakisema ni Carol.. kesi ingekuwa ukweli ningefungwa maisha," alisema.

Alipoewa nafasi ya kunena maneno ya mwisho kwa mama mkwewe, Erick alisema, "Nawapenda kabisa, kabisa. Singependa uniache. Nikipiga simu naomba ushike."

Mama Carol alisisitiza kwamba atangoja kusikia msimamo wa binti yake ili wajue hatua ya kuchukua.