Patanisho: Caretaker wa kanisa aachwa baada ya pasta kumfumania na mwanadada mwingine kanisani

Benson alisema mkewe alitoroka baada ya yeye kufumaniwa na mwanadada mwingine kanisani ambako anafanya kazi.

Muhtasari

•Benson alisema ndoa yao ya miaka sita imekabiliwa na changamoto si haba kwani bado hawajafanikiwa kupata mtoto pamoja.

•Faith alidai kuwa mpenzi huyo wake amekuwa akienda nje ya ndoa kwa miaka yote ambayo wamechumbiana.

Image: RADIO JAMBO

Benson Ngeno ,30, kutoka Nakuru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Faith Kipkorir ambaye alimuacha mwezi uliopita.

Benson alisema ndoa yao ya miaka sita imekabiliwa na changamoto si haba kwani bado hawajafanikiwa kupata mtoto pamoja.

"Tulikosana mwezi uliopita. Tumeoana miaka sita. Hatujawahi kupata mtoto. Nilimuoa na mtoto mmoja. Kuna msukumo kwa wazazi kwa nini mke wangu hazai," Benson alisema.

Benson alifichua kuwa mkewe alitoroka baada ya yeye kufumaniwa na mwanadada mwingine kanisani ambako anafanya kazi ya kusimamia mali.

"Nikiwa kazini pale kanisani, nilileta mwanamke, kwa bahati mbaya au mzuri pasta akanipata. Hiyo ilimkasirisha mke wangu sana. Nilifutwa kazi pale kanisani nikafukuzwa. Mke wangu alikasirika akaenda. Nilimpigia juzi lakini kuskia sauti yangu akaniweka blacklist," alisema.

Aliongeza, "Ndio nilete mwanamke mwingine nilikuwa nimesema nijaribu nione kama ni mimi niko na shida. Hatujaweza kumuona daktari. Nilikosea ndio maana nilikuwa nataka kuomba msamaha. Sijaweza kuenda kwao. Vile ameniblacklist imekuwa ngumu sana hata kuenda kwao. Wako na shida ya network huko kwao."

Faith alipopigiwa simu alidai kuwa mpenzi huyo wake amekuwa akienda nje ya ndoa kwa miaka yote ambayo wamechumbiana.

Aidha, aliweka wazi kuwa tayari amemtema kabisa jamaa huyo na kumtaka aendelee na maisha yake.

"Hiyo ni uongo tupu. Hiyo amesema kuhusu wanawake huwa anafanya miaka yote tumeishi naye. Kwanza alipatwa na pasta. Nimevumilia sana na huyo jamaa sana lakini sasa nimefika mwisho. Nimemuacha kabisa.," alisema.

Kuhusu suala la wao kutopata mtoto, Faith alisema kuwa ulikuwa uamuzi wake mwenyewe kwa sababu zake binafsi.

"Mimi mwenyewe nilifanya uamuzi. Nilimwambia ameishi kunifanyia hivyo. Hajawahi kufika kwetu na anataka nimzalie," alisema.

Benson aliendelea kuomba msamaha na kumsihi mpenzi huyo wake warudiane ila maombi yake yaliangukia masikio yenye pamba.

"Sina uhusiano tena na wewe. Na uachane na mimi. Wee endelea na maisha yako na wanawake wako. Mimi nilee mtoto wangu. Nimekusamehe mara ngapi? Wewe endelea na maisha yako," Faith alimwambia Benson.

Kufuatia hayo, Benson hakuwa na budi ila kukubali uamuzi wa mwanadada huyo ambaye alisema tayari amepata mwingine.

"Nimekubali yale umeamua. Lakini nilikupenda na nitaendelea kukupenda," alisema.

Faith alisema, "Yeye tu aendelee na maisha yake."