Patanisho: Mke wa pili atoroka na kumuachia mumewe watoto wawili ambao aliolewa nao

Mary alitoa masharti ya yeye kurudi ambapo aliai David alipe karo ya wanawe ya sekondari na amjengee nyumba.

Muhtasari

•David alikiri kuwa ana mke mwingine nyumbani na kudai kuwa Mary anafahamiana na familia yake nyingine.

•Mary alisema sababu ya yeye kuondoka na kuacha watoto wake ilikuwa kwa sababu alitaka kuwatafutia karo ya sekondari.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho kwenye Gidi na Ghost Asubuhi, David Asalimba mwenye umri wa miaka 40 kutoka Huruma, Nairobi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mary Muhanja mwenye umri wa miaka 35.

David alisema amekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu ndoa yake ya miaka minne tangu mke wake alipoondoka na kumuachia watoto wake wawili ambao alikuja nao. Alisema kwamba hawajafanikiwa kupata mtoto pamoja.

"Tulipatana na mke wangu miaka 4 imepita. Alikuwa rafiki yangu shuleni.Alisema anaenda kazi ya salon. Alinipigia simu akasema anakuja, baadaye akaniambia kwamba anasaidia rafiki yake ambaye amezaa. Hapo awali alikuwa ameniweka blacklist, amenifungulia simu hivi majuzi. Tukiongea anasema atarudi. Kila wakati anasema atarusi next week. Next week ikifika harudi. Sijui ako wapi," David alisema.

David aliendelea kukiri kuwa ana mke mwingine nyumbani na kudai kuwa Mary anafahamiana na familia yake nyingine.

"Nikipiga simu yake haikuwa inaingia. Kakangu alimuongelesha akawa tunaongea. Ameenda mwezi moja siku tatu. Watoto ambao aliniachia ni watoto alikuja nao. Niko na mke mwingine, yeye ni wa pili. Alikuwa amesema ameenda kazi. Sasa amebadilika. Alikuwa anasema anataka kuongea na mama na baba. Lakini ameongea na ndugu zangu.Mahitaji ya watoto nashughulikia. Karo ananisaidia. Mke wa kwanza ako nyumbani. Anamjua huyu. Ata huyu nilimwambia niko na bibi," alisema David.

Mary alipopigiwa simu alikiri kwamba ni kweli aliondoka na kuenda kutafuta riziki.

Hata hivyo alisisitiza kwamba sababu ya yeye kuondoka na kumuachia mumewe watoto wake ilikuwa kwa sababu alitaka kuwatafutia karo ya sekondari.Pia alitilia shaka ndoa yake na David akilalamika kuwa hajatambulishwa nyumbani.

"Hajawadanganya. Niko kazi. Yeye hana kazi. Ilibidi ning'ang'ane na kazi. Ako na bibi na watoto wanne. Muda mrefu amekuwa hana kazi. Niko na watoto wawili ambao wanaingia sekondari. Ilibidi ning'ang'ane nitafute mwenyewe. Mtu hanipeleki kwao sijui kama mimi ni mke ama ni rafiki wa Nairobi," Mary alisema.

Aliongeza, "Kuna mahali alikuwa ananisaidia lakini mara nyingi ananiambia hana kazi. Wakati mwingi anashughulikia familia yake. Ako na watoto wawili katika sekondari na wanamhitaji. Nilimwambia ashughulike na watoto wake kwanza. Sijawahi kuona ameniunganisha na familia yake na bibi yake. Hata watoto wake. Nilimuona mke wake mara moja tu. Miaka mitatu tumekaa na yeye na hajanitambulisha kwa familia. Huwa anaenda nyumbani anarudi baada ya siku chache. Anakaa na mimi kuliko bibi yake nyumbani."

David alimwambia mkewe, "Ukae ukijua bado nakupenda. Tulipendana tangu tukiwa shule. Hata ungekuwa bibi wa kwanza si wa pili. Najua Corona ilikuja shida ikaingia. Lakini  nakupenda na ya Mungu huyajui."

Mary alimlalamikia, "Kama uko na watoto uko na shida gani? Niliambia watoto nimeachana na baba yao? Kwa nini unanisomea kwa Kenya mzima? Nimekuwa nikikulilia unipeleke kwa mama yako na baba yako hujawahi kunipeleka, Saa hii ndo unataka? Umenificha huwezi kunionyesha kwa baba yako. Unaniambia ile wakati nitabadilisha tabia zangu ndio utanipeleka. Saa hii tabia haijabadilika.'

Mama huyo wa watoto wawili aliendelea kutoa masharti ya yeye kurudi na kudai David alipe karo ya wanawe na amjengee.

"Naporudi, anaenda kuingiza watoto shule?  Akipeleka watoto shule na anijengee mimi nitarudi. Baada ya mimi kuondoka umeanza kuwa mzuri mzuri umeiva iva. Ukiendelea kuwa mzuri hivyo mambo yatakuwa sawa... Una pesa ngapi unitumie nikuje hapo tuongee? Niko na shughuli nyingi nataka kufanya. Tuma hiyo hela nikuje," Mary alimwambia mumewe.

Licha ya David kukiri waziwazi kumpenda sana, Mary alibainisha kuwa mapenzi yake kwake huwa ya msimu tu.

"Gidi, wewe unaweza ishi na mtu vipi kama hakuna mapenzi? Kuna mahali vituko inakuwa zaidi mapenzi yanaenda," alisema Mary.

Aliongeza, "Mimi niko kazi. Nimekuwa nikitafutia watoto wangu. Kurejea narejea. Kwanza anipeleke kwao nikae na wazazi wake na bibi yake."

Alipopewa fursa ya kumwambia mkewe maneno ya mwisho, David alimwambia, "Mi nakupenda sana. Hata wewe unajua nakupenda kutoka juu hadi juu. Bila wewe sioni maisha yangu yakikaa sawa. Kama nilikukosea mahali naomba msamaha."

Mary alisema,"Mimi sina shida sijui nimwambie vipi. Nitaongea naye mwenyewe."

Je, ushauri wako kwa wawili hao ni upi?