Patanisho: Mama alinitupa barabarani nikiwa na miaka 3 ili gari ikuje nigonge- Jamaa asimulia

Stanley alikiri kumtusi mzazi huyo wake baada ya kutofautiana, hatua ambayo ilizidisha ugomvi baina yao.

Muhtasari

•Stanley alisema uhusiano wake na mamake uliharibika mwaka wa 2021 baada ya wao kuzozana kuhusu masomo.

•Bi Omanji alipopigiwa simu, alikanusha baadhi ya madai ya mwanawe na kuweka wazi kwamba alikataa masomo.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Stanley Andera ,21, kutoka Kimilili alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake mzazi Wilkister Omanji ambaye alitofautiana naye takriban miaka miwili iliyopita.

Stanley alisema uhusiano wake na mamake uliharibika mwaka wa 2021 baada ya wao kuzozana kuhusu masomo.

"Sikulelewa na yeye. Mwaka wa 2019, aliniita niende huko nisomee huko.Baada ya kumaliza class 8, hakutaka niingie form 1. Alitaka niende welding lakini sikutaka. Nilisoma kidogo alafu karo ikakosekana. Nikatoroka shule nikaenda kutafuta kazi," Stanley alisimulia.

Stanley pia alikiri kumtusi mzazi huyo wake baada ya kutofautiana, hatua ambayo ilizidisha ugomvi baina yao.

"Kuna message nilimwandikia nikimtusi . Alisema nisiwahi kumuongelesha. Hivi majuzi aliniita lakini hakuniongelesha vizuri. Alisema hata nikifanya kazi, pesa itakuwa ikapotea sitawahi kushika kitu kwa mikono. Nilikuwa nataka anifungue," alisema.

Aidha, aliibua madai kwamba mzazi huyo wake alikuwa amemtupa akiwa na mdogo na akalazimika kulelewa na nyanya yake.

"Nilitupwa nikiwa na miaka mitatu. Alinitupa kwa nyanya yangu wa pande ya baba. Niliambiwa ati alinitupa kwa barabara gari ikuje inigonge, watu wakanichukua wakanipeleka kwa nyanya yangu nikalelewa na yeye na shangazi yangu... Ningependa anifungulie roho. Sina amani kwa roho yangu," Stanley alisimulia.

Bi Omanji alipopigiwa simu, alikanusha baadhi ya madai ya mwanawe na kuweka wazi kwamba alikataa masomo.

Aliendelea kumuagiza kijana huyo afunge safari hadi nyumbani ili kuomba msamaha kwa njia ya ana kwa ana.

"Mimi sipendi uongo. Nimemuita juzi akuje na mwenzake. Alishindwa kuniongelesha. Alikataa shule, akakataa welding, akakataa driving na akakataa shule. Sijui kwa nini ameniweka hewani. Apande gari akuje.. Sitaki aniweke hewani. Nimeokoka asiniharibie jina," Bi Omanji alisema kabla ya kukata simu.

Stanley alisema, "Mama ni mkali, hawezi kuelewa maneno. Alikataa kulipa karo kwa sule na walimu hawakuwa wanaelewa."

Alipopewa fursa ya kunena na mzazi huyo wake hewani, alimwambia, "Mama naomba unifungue tu. Kubali tu ufungue roho yako nikae na amani."