Patanisho: Mwanadada agundua mumewe ana mke mwingine na mtoto baada ya miaka 3 ya ndoa

Moraa alisema tabia ya mumewe ilianza kubadilika baada ya mtoto wao kuzaliwa hadi akachukua hatua ya kutoroka.

Muhtasari

•Moraa alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilianza kuyumba baada ya yeye kupata ujauzito kisha akagundua mumewe ana mke mwingine.

•Steve alipopigiwa simu, mwanzoni alizungumza vizuri sana hadi wakati Gidi alipomwambia angependa kumpatanisha na Moraa.

 

Image: RADIO JAMBO

Mwanadada aliyejitambulisha kama Rebecca Moraa ,24, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mpenzi wake Steve Mogire ,32, ambaye alikosana naye takriban mwezi mmoja uliopita.

Moraa alisema ndoa yake ya miaka mitatu ilianza kuyumba baada ya yeye kupata ujauzito kisha akagundua mumewe ana mke mwingine.

"Tulipatana na yeye tukaka vizuri bila maneno. Wakati alinipea mimba akaanza kuhepa. Nilienda kukaa nyumbani. Nikazaa nikiwa kwa mama. Nilipozaa alikuja akanibembeleza nimpelekee mtoto. Nikampeleka mtoto akiwa na miezi miwili," Moraa alisimulia.

Moraa alifunguka jinsi tabia ya mumewe ilianza kubadilika ghafla baada ya mtoto wao kuzaliwa hadi akachukua hatua ya kutoroka.

"Sikujua ako na bibi, nilikuja kujua baadaye ako na bibi kupitia kwa rafiki yake. Sijui bibi yake ako wapi. Alianza kunitesa. Alianza kukosa kushughulikia mtoto tukiwa na yeye. Alianza kuongea na wasichana kwa simu. Nikamuuliza mbona hakuniambia ako na familia nyingine. Hapo ndio ilileta maneno nikatoka nikaenda," alisema.

Aliongeza, "Nataka kumuomba msamaha kwa sababu wakati nilimpata akiongea na wasichana nikamuongelesha vibaya nikamwambia akae na hao wasichana wake. Hapo mwanzo tulikuwa tunaishi na yeye. Niliona tunaishi vizuri nikadhani itakuwa hivyo."

Steve alipopigiwa simu, mwanzoni alizungumza vizuri sana hadi wakati Gidi alipomwambia angependa kumpatanisha na Moraa ambapo alisema, "Kidogo, kidogo, niko mahali kuna kelele..." kisha akakata simu.

Moraa alisema, "Ningependa tu turudiane tuishi vile tulikuwa tunaishi. Niliongea na mamake akasema huyo bibi mwingine ako Nairobi. Naomba aweze kupanga turudiane na yeye na anisamehe kwa yale maneno nilimwambia."

Je, una maoni yapi kuhusu Patanisho ya leo?