Patanisho: Jamaa arukwa baada ya kudai mkewe alimpiga mamake na kumuachia mtoto wa miezi 4

"Sina mtoto na yeye. Sijawai kuzaa mtoto naye. Sijawahi hata kupata mimba," Patricia alisema.

Muhtasari

•Albert alidai kuwa mke wake aligura ndoa yao takriban miezi miwili iliyopita na kumuachia mama yake mtoto wa miezi minne.

•Patricia alisema kwa kuangazia sauti ya jamaa huyo alisikia kama kwamba ni jirani yake anayejulikana kwa jina Kelly.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Jamaa aliyejitambulisha kama Albert Wafula kutoka Gatukuyu aligunduliwa kuwa muongo baada ya kutuma ombi la kupataniushwa na Bi Patricia Okumu ambaye alidai ni mke wake na mama ya wanawe wawili.

Albert ambaye baadaye ilibainika anaitwa Kelly alidai kuwa mke wake aligura ndoa yao takriban miezi miwili iliyopita na kumuachia mama yake mtoto wa miezi minne.

Alidai kuwa mkewe alikuwa na mazoea ya kutoroka toroka kila mara akiwa kazini kabla ya kutoweka kabisa hatimaye.

"Mke wangu ni mtu wa kutorokatoroka kila saa, sio mtu wa kutulia. Nilikuwa kazini nikaskia ameacha mtoto. Nilijaribu kufuatilia lakini hatukuelewana," Albert alidai.

Aliongeza, "Alikuja kukosana na mama yangu kidogo na akampiga. Kuenda nyumbani nilipata ametoroka. Aliacha mtoto wa miezi minne. Nilibaki kumpatia maziwa tu.Alienda na huyo mtoto mwingine mkubwa.  Alikuja Nairobi miezi miwili ilipita. Hatujapatana. Tumezungumza siku moja lakini hatukuelewana."

Albert alidai kuwa mkewe alihamia jijini Nairobi baada ya kutoroka nyumbani.

Bi Patricia alipopigiwa simu alibainisha kuwa hamfahamu Albert. Aliweka wazi kwamba kwa kuangazia sauti ya jamaa huyo alisikia kama kwamba ni jirani yake anayejulikana kwa jina Kelly.

"Naskia kama ni Kelly.Hiyo jina amedanganya. Ni kaboy ka hapo kwetu. Kalikuwa kananitongoza tu shule ile ya kucheza. Ni juzi tu nilimtumia friend request kwenye Facebook. Amedanganya, anaitwa Kelly. Ni muongo," Patricia alisema.

Aidha alipuuzilia mbali kuwa na watoto na jamaa huyo huku akiweka wazi kwamba hata hajawahi kuwa mjamzito.

"Sina mtoto na yeye. Sijawai kuzaa mtoto naye. Sijawahi hata kupata mimba. Sijawahi kubeba mimba yake ata sijawahi kutoa mimba," alisema.

Baada ya kugundua amepatikana, Albert alikata simu mara moja bila hata kujibu madai ambayo yaliibuliwa na Patricia.

Je, una maoni yapi kuhusu mwanamke kumpiga mama mkwe?