Patanisho: Mwanadada alia baada ya kugundua jamaa aliyemdanganya mkewe alifariki ana familia

Raia huyo wa Rwanda alisema mambo yalibadilika alipoenda nyumbani kwa mchumba wake ambapo alipata viatu vya mwanamke.

Muhtasari

•Bi Zawadi alisema mahusiano yalivunjika baada ya kushika mimba na mchumba wake kumshauri atoe, hatua ambayo hakutaka kuchukua.

•Bi Zawadi alisema licha ya kugundua kwamba mchumba wake ana mke mwingine, yuko tayari kuwa mke wa pili.

Image: RADIO JAMBO

Alhamisi asubuhi, mwanadada aliyejitambulisha kama Zawadi Mambuwa mwenye umri wa miaka 24 alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Patrick Makau ,34, ambaye alikosana naye hivi majuzi.

Bi Zawadi alisema mahusiano yao ya chini ya mwaka mmoja yalivunjika baada ya kushika mimba na mchumba wake kumshauri atoe, hatua ambayo hakutaka kuchukua.

"Gidi niko na shida kubwa ambayo inafaa ikaliwe na wazee. Nimekuwa na mwanaume kwa mahusiano. Aliniambia hajawahi kuoa. Na mimi nikakubali. Aliniambia mwenye alifaa kukaa naye alikufa akaona hakuna haja ya kuoa.

Baadae alinionyesha marafiki zake na akawaambia kuwamimi ndio bibi yake. Mimi sio Mkenya. Mimi ni Mnyarwanda," Zawadi alisimulia.

Raia huyo wa Rwanda alisema mambo yalibadilika wakati alienda nyumbani kwa mchumba wake ambapo alipata viatu vya mwanamke.

Makau hata hivyo alibainisha kuwa ni vya dadake ambaye humtembelea  mara kwa mara, madai ambayo Zawadi alikuja kugundua ni uongo.

"Wakati nilikuwa kwake niliona viatu za mwanadada. Nikamuuliza akasema ni dadake huwa anakuja kumtembelea. Kidogo kidogo vile nilipata mimba akataka nitoe. Nikaona hapana juu mahali naishi ni kwa wenyewe. Huwa nafanyia mwanamke mwingine kazi," alisema.

Aliendelea, "Saa hii nikimpigia simu hashiki. Nilienda kutafuta huyo dadake. Niligundua kumbe  ni mtu ambaye alikuwa na familia yake na wanaishi hapo. Nilipata mtoto nikamuuliza baba yake ni nani akasema ni huyo mume wangu. Saa hii nashindwa nifanye nini. Mimi sikutaka kuharibu ndoa ya mtu. Juu bibi yake akijua itakuwa shida. Tena hashiki simu zangu."

Bi Zawadi alisema licha ya kugundua kwamba mchumba wake ana mke mwingine, yuko tayari kuwa mke wa pili.

"Angekubali kunichukua kama mke singekataa, lakini ajulishe mke wake. Alijua niko na mtoto mwingine, akanidanganya atanioa. Niko na mtoto mwingine mdogo," alisema. 

"Tulijuana na huyo jamaa mwaka wa 2020. Nilikuwa na customer yake lakini hakuwa ameniambia. Juzi juzi nikaskia simu imeitana. Akaniambia tukutane. Akaniambia amenisamehe kwa kupata. Nikamwambia sijaolewa. Na yeye akaniambia hajaoa," aliongeza.

Aliendelea, "Tulikuwa na yeye wiki iliyopita. Nikamwambia sitaki kuharibu familia yake, anioe kama mke wa pili lakini afahamishe bibi yake.Naogopa kuongea na mke wake nisije nikapigwa."

Kwa bahati mbaya, Bi Zawadi hakuweza kupatanishwa na mchumba wake kwa kuwa Bw Makau hakuchukua simu alipopigiwa.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisikika kulemewa na hisia na akachukua hatua ya kufanya dunia huku akilia.

"Nishike mkono Bwana. Mimi sina la kufanya. Nyumbani ni mbali na hata sina nauli ya kufika. Ni uchungu, sijui watoto wawili nitalea aje.." aliomba.

Je, una ushauri upi kwa mwanadada huyo?