Patanisho: Mume ampiga mkewe baada ya kuambiwa anauza pombe ndani ya nyumba yao

Faith alilalamika kuwa mumewe amepeleka mwanamke mwingine kwa nyumba yake miezi miwili tu baada ya kumfukuza.

Muhtasari

•Faith alisema ndoa yake ya miaka 14 ilisambaratika baada ya mumewe kumfukuza nyumbani na kumwambia asiwahi kurudi.

• "Kama nilimkosea, naomba anisamehee nirudi nilee watoto wangu. Na kama hataki ni sawa tu," alisema Faith.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Faith Amojong ,30, kutoka Kitale alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Philip Simiyu ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Faith alisema ndoa yake ya miaka 14 ilisambaratika baada ya mumewe kumfukuza nyumbani na kumwambia asiwahi kurudi.

"Bwanangu ni mtu anapenda kuskia maneno ya watu. Akiambiwa kitu nje hakuskizi anakuja tu kukuchapa.  Aliambiwa ati mimi huwa nauza pombe kwa nyumba yake. Badala akuje kuniuliza akakuja akanipiga. Ni kitu amezoea. Ni mwanaume anapenda kutembea na wanawake, lakini ananishuku mimi ndio natembea na wanaume. Hata huwezi enda mahali, ukienda hata kanisani anakushuku,"  Faith alisema.

Aliendelea, "Nimevumilia miaka 14 sababu tu ya watoto. Nataka turudiane juu ya watoto. Yeye ndiye alinifukuza. Watoto wanapiga simu wanasema wanashindwa vile watasoma. Nikimpigia simu hashiki. Aliniambia niende na nisiwahi kurudi. Siwezi jua ni kwa sababu ya hasira ama ni nini. Kama ni kurudi labda niende nichukue chief tuende na yeye."

Faith alidai kwamba mumewe tayari amepeleka mwanamke mwingine kwa nyumba yake miezi miwili tu baada ya kumfukuza.

"Ako na mwanamke mwingine. Amemleta nyumbani, wanatoka asubuhi wanarudi jioni. Ni kama hashughulikii watoto. Nikipiga simu watoto wananiambia kuna mwanamke mwingine. Nilikuwa naona niende kwa chifu nichukue watoto niende nao," alisema.

Juhudi za kumpatanisha Faith na mumewe hata hivyo ziligonga mwamba kwani Bw Simiyu hakushika simu yake alipopigiwa.

Faith alimalizia kwa kusema, "Kama nilimkosea, naomba anisamehee nirudi nilee watoto wangu. Na kama hataki ni sawa tu."